25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Polisi Musoma watuhumiwa kuua raia

MWANDISHI WETU -Musoma

MKAZI wa Kijiji cha Busegwe, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Anthony Lushete, maarufu DJ Anthony D.O.B (25), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na polisi waliomchukua kazini kwake katika klabu ya usiku ya Modern, barabara ya Iringo mjini Musoma.

Taarifa ambazo MTANZANIA imezipata zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari 14, mwaka huu – Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day). Pia vijana kadhaa katika klabu hiyo walikamatwa.

Inadaiwa siku ya tukio, vijana hao wakiwa kazini, askari polisi wanane wakiwa na rafiki zao wa kike walifika eneo hilo na kutaka kuingia disko bila kulipa kiingilio jambo ambalo mlinzi wa klabu hiyo hakuliafiki na kuzua mvutano kati yao.

Chanzo cha habari kilieleza kuwa baada ya mlinzi huyo kuwagomea, askari hao walitumia nguvu wakitaka kuingia na kuanza kumshambulia kwa mateke na ngumi.

Kwamba baada ya kutokea hali hiyo, Lushete alikimbia mlangoni hapo kuamulia ugomvi huo na kumtetea mfanyakazi mwenzake, lakini alikamatwa na polisi hao, wakaondoka naye. Alishikiliwa kuanzia siku hiyo hadi Februari 26, alipofariki dunia.

Chanzo kilisema licha ya wenzake kutembelea vituo mbalimbali vya polisi, kikiwamo kituo kikuu cha mjini Musoma, walielezwa hayupo, lakini walishangaa baadaye kuelezwa  anashikiliwa kituoni hapo kwa tuhuma za wizi wa kompyuta mpakato – laptop.

“DJ Lushete alifungiwa kituo cha polisi na kuanza kupigwa kuanzia tarehe 14 bila dhamana wala kuwajulisha ndugu zake ambao walifanya jitihada za kumtafuta kila kituo cha polisi, na cha ajabu ni kwamba alikuwa hapo hapo Central Police Musoma mjini amefichwa na kuendelea kubambikiwa kesi,” kilieleza chanzo hicho.

Mmoja wa vijana ambao walikuwa wakishikiliwa kituoni hapo, alisema Februari 25, mwaka huu alipokamatwa kwa kosa la kutovaa kofia nguvu na kupelekwa kituoni hapo, alimkuta Lushete akiwa na hali mbaya, huku amefungiwa chumba cha peke yake na ilipofika usiku walizimiwa taa, baadae wakaona anaondolewa.

“Alikuwa anahangaikia uhai, hali yake ilikuwa mbaya kwa kweli maana tulikuwa tunamchungulia kwa sababu zile selo ukimchungulia unamwona, basi ikawa imefika usiku yakawa yanatokea mazingira ya ajabu, taa zinazimwa, zinawashwa, tukawa tumeshituana tunyamaze, tukasikia mtu anatolewa, tukajua ni yeye.

“Hata wale waliokuwa wametuletea chakula walituambia hata taa za nje zilizimwa na waliona mtu anapandishwa kwenye gari, kesho yake nilipofuatilia nikaambiwa ni yeye kwa sababu nilimpigia simu mwenzangu kufahamu kama amemwona akasema amekwenda polisi hajamkuta.

 “Nikamsilimulia hali ilivyokuwa ndiyo akachukua hatua ya kwenda, kila akiwaambia amepeleka chakula wanamkwepa, hata barua ya dhamana hawakupokea, akawa amejiongeza akaenda mochwari akakuta dogo amekufa,” alisema rafiki yake huyo.

Chanzo kingine kilieleza kuwa jambo lililowashtua ni mazishi yake kufanyika chini ya ulinzi wa polisi waliokuwa wamemsindikiza baba yake mzazi wakiwa wamejihami kwa silaha za moto na mabomu ya machozi. Baadhi ya askari walikwenda msibani na wengine wakabaki barabarani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Alfred Shila, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema halifahamu na ndiyo analisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwa mwandishi wa habari hizi.

Kamanda Shila alionyesha kushangazwa na kitendo cha baba mzazi wa Lushete (jina tunalo) kushindwa kuwasiliana naye kuhusu tukio hilo licha ya kuwa yeye ni mwajiriwa wa jeshi hilo.

“Ndiyo unanieleza wewe, sina hiyo taarifa, baba yake umesema ni askari, kwanini anashindwa kuniona mimi? Hizo taarifa mimi sina, mshauri huyo mzazi aje anione mimi,” alisema Kamanda Shila.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles