BADI MCHOMOLO NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
NYOTA wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagle), Nwankwo Kanu, amewataka wachezaji wa Tanzania kujituma kutokana na umri wao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye aliwahi kukipiga katika klabu ya Arsenal, yupo nchini kwa ziara maalumu na kampuni ya Star Times.
Akifanya mazungumzo na kituo kimoja cha Radio hapa nchini, Kanu alisema anaamini kuna vijana wengi wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka, hivyo wanatakiwa kujituma kutokana na umri wao ili waweze kufanikiwa.
“Najua Tanzania kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka, lakini ili wafanikiwe wanatakiwa kujituma zaidi, hasa kutokana na umri wao.
“Ninaamini kuna wachezaji wengi ambao wana lengo la kwenda kucheza soka Ulaya, wanaweza kupata nafasi ya kucheza kama wana vipaji na umri ukiwa mdogo ili waweze kuzitumikia klabu kwa kipindi kirefu,” alisema Kanu.
Mchezaji huyo amewataka wachezaji wa Tanzania kutengeneza mazingira ya urafiki na wachezaji wa mataifa mbalimbali kwa njia ya mitandao ili kuweza kubadilishana mawazo katika soka.
“Ulaya wachezaji wanapenda kutengeneza urafiki wa karibu kwa ajili ya kubadilishana mawazo katika soka, hivyo wachezaji wa Tanzania nao wanatakiwa kufanya hivyo kwa ajili ya kubadilishana mawazo, itawasaidia,” aliongeza Kanu.
Wakati huo huo, Kanu jana alitembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo alieleza atahakikisha anawasaidia wagonjwa wenye matatizo ya moyo nchini kila mwezi ili warudishe matumaini ya maisha yao.
Mchezaji huyo, akiwa kwenye Taasisi hiyo, alitoa msaada wa sabuni zenye thamani ya Sh milioni 10 kama sehemu ya kuwafariji.
Kanu alisema kupata tatizo hilo si sababu ya kupoteza matumaini ya kuishi, kwani mgonjwa anaweza kuishi miaka mingi zaidi na kukamilisha ndoto zake.
“Nikiwa bado nacheza mpira mwaka 1999, nilifanyiwa upasuaji wa moyo nchini Marekani, sikukata tamaa, nilipopona niliendelea na kazi yangu hiyo kwa miaka 12 zaidi kabla sijastaafu, nawaomba wagonjwa wasikate tamaa, lengo la ziara yangu hapa nchini ni kuwapa moyo wakati najipanga kuona namna nitakavyoweza kuwasaidia baadhi ya wagonjwa kila mwezi ili wapatiwe matibabu,” alisema.
Alisema kutokana na kuwepo na changamoto ya hospitali za moyo, kwa kushirikiana na kampuni ya Star Times, kama balozi wao wataangalia namna ya kutengeneza kituo kimoja hapa nchini ambacho kitakuwa kikitoa huduma hizo.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa upasuaji moyo kwa watoto, Godwin Sharaw, alisema wamefarijika kwa ujio wa mchezaji huyo na iwe changamoto kwa wachezaji wengine kujitokeza kufariji wagonjwa na hata wao kufanya uchunguzi wa mioyo yao.
“Baadhi ya wagonjwa tulipowafahamisha ujio wa mchezaji huyu walionekana kufurahi na kukaa wakimsubiri kwa hamu, tuna imani walipomuona na kuwapa historia yake imewasaidia kuwafariji, nadhani kama wapo waliokata tamaa watarejesha matumaini,” alisema.