Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WATOTO kati ya 100 hadi 150 kila mwaka nchini hufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kupatiwa matibabu dhidi ya ugonjwa wa saratani ya jicho.
Takwimu hizo zilitolewa jana Dar es Salaam na Dk. Anna Sanyiwa wa MNH Kitengo cha Saratani wakati alipozungumza na MTANZANIA juu ya maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya jicho kwa watoto.
“Maadhimisho haya hufanyika kuanzia Mei 8 hadi 15 kila mwaka yakiwa na lengo la kupeleka elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huu. Hapa Muhimbili tumekuwa tukipokea watoto kati ya 100 hadi 150 kila mwaka wenye tatizo hili ambalo kitaalamu linajulikana kama ‘Retinoblastoma,” alisema.
Alifafanua kuwa saratani hiyo hutokana na hitilafu inayotokea kwenye vinasaba (genetic defect) ambayo huathiri katika utando wa fahamu wa jicho, na kwamba huanza kujitokeza baada ya miaka mitatu ya uhai wa mtoto tangu alipozaliwa.
“Hata hivyo mara chache sana hujitokeza baada ya miaka mitano. Saratani hii huwapata watoto wa jinsi zote kwani inahusisha vinasaba, yaani inarithiwa. Kuna uwezekano wa asilimia 50 ya familia yenye vinasaba hivi kupata mtoto mwenye ugonjwa huu.
“Takwimu zinaonyesha pia asilimia 60 ya watoto wanaorithi vinasaba hivyo hupoteza macho yao yote mawili, lakini asilimia 40 huathirika jicho moja, hasa wale ambao wazazi wao huwa wameoana huku wakiwa ni ndugu wa karibu,” alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu hadi minne iliyopita, wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka Kanda ya Ziwa.
“Takwimu zetu zinaonyesha hivyo, lakini bado tunaendelea kuzichambua na hata kuangalia kwanini wengi wanatokea katika kanda hiyo kuliko kanda nyingine hapa nchini,” alisema.
Dk. Sanyiwa alisema mara nyingi dalili za ugonjwa huo huwa zinafanana kwa karibu na dalili za magonjwa mengine ya macho, na kwamba daktari bingwa wa macho ndiye anaweza kuangalia na kutofautisha saratani na magonjwa mengine.
“Dalili zenyewe hutegemea hatua ya ugonjwa, hata hivyo dalili za mwanzo huwa ni jicho kuonyesha weupe kwenye mboni, mtoto wa jicho, jicho kuwaka kama paka usiku au mwanga mweupe ukipiga picha na ‘flash’,” alisema.
Alitaja dalili nyingine kuwa ni kengeza, weupe kwenye kioo cha jicho, jicho kuvilia damu, kuwa jekundu na kuuma.
“Dalili nyingine hutokea ugonjwa unapoendelea kukomaa kwa mfano hufika mahali hadi jicho linakuwa kubwa na kuvimba,” alisema.
Daktari huyo aliwashauri wazazi kuwafikisha watoto mapema hospitali pindi wanapoona dalili za aina hiyo.
“Mbali na Hospitali ya Taifa Muhimbili, bado kuna vitengo vingine vya macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) pamoja na Bugando, Mwanza,” alisema.