Esther Mbussi na Adam Mkwepu, Dar es Salaam
SHULE za msingi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa zimeongoza matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2014 kwa kushika namba moja hadi saba kati ya shule 10 bora kitaifa.
Aidha, watahiniwa wamefaulu zaidi somo la Kiswahili na kufeli zaidi somo la Hisabati.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE), wavulana wameongoza somo la Hisabati kwa kupata alama 50/50, ambapo 26 wamefaulu kwa kiwango hicho na wasichana wakiwa wanane.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alizitaja shule 10 bora kuwa ni Twibhoki ya Mara ambayo imeshika nafasi ya kwanza, Mugini iliyoshika nafasi ya pili, Peace land na Alliance zote za Mwanza, Kwema (Shinyanga), St. Severine (Kagera), Rocken Hill (Shinyanga), Tusiime (Dar es Salaam), Imani (Kilimanjaro) na Palikas (Shinyanga).
“Kwa upande wa mikoa iliyofanya vizuri kitaifa na asilimia zake za ufaulu kwenye mabano ni Dar es Salaam (46,434), Kilimanjaro (26,192), Mwanza (37,017), Iringa (14,650), Arusha (23,250), Tanga (26,261), Njombe (11,389), Kagera (24,501), Geita (17,560) na Mtwara (15,608).
“Wilaya zilizoongoza kitaifa ni Mpanda Mji (Katavi), Biharamulo (Kagera), Moshi (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Arusha (Arusha), Kinondoni (Dar es Salaam), Korogwe Vijijini (Tanga), Ilala (Dar es Salaam), Iringa (Iringa) na Mji Makambako (Njombe),” alisema Dk. Msonde.
Akizungumzia ufaulu wa kimasomo, alisema katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.64 na 8.94 ikilinganishwa na mwaka jana.
“Watahiniwa wamefaulu zaidi somo la Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 69.70 tofauti na asilimia 69.06 ya mwaka jana, na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini zaidi ni Hisabati lenye ufaulu wa asilimia 37.56 ambapo mwaka jana ilikuwa ni asilimia 28.62.
“Katika somo la Kiingereza watahiniwa waliofaulu kwa mwaka huu ni asilimia 38.84 ikilinganishwa na mwaka jana asilimia 35.52 na Sayansi kwa mwaka huu waliofaulu ni asilimia 54.89 na mwaka jana asilimia 47.49,” alisema.
Dk. Msonde alisema jumla ya watahiniwa 451,392 kati ya 792,118 waliofanya mtihani huo wamepata alama 100 au zaidi katika alama 250 ambapo idadi hiyo ni sawa na asilimia 56.99.
Alisema kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 226,483 ambao ni sawa na asilimia 53.59 na wavulana ni 224,909 sawa na asilimia 60.87.
Miongoni mwa watahiniwa hao waliofaulu, Dk. Msonde alisema wamo wenye ulemavu 795 wakiwamo wasichana 355 ambao ni sawa na asilimia 44.65 na wavulana 440 ambao ni sawa na asilimia 55.35.
“Katika mtihani huo uliofanyika Septemba 10 na 11, mwaka huu jumla ya watahiniwa 808,085 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 429,624 sawa na asilimia 53.17 na wavulana 378,461 sawa na asilimia 46.83.
“Kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 691 walikuwa na uoni hafifu, 87 walikuwa na ulemavu wa macho (wasioona), wenye matatizo ya kusikia 374, wenye mtindio wa ubongo 252 na watahiniwa 27 walikuwa na ulemavu zaidi ya mmoja,” alisema Dk. Msonde.
Pamoja na mambo mengine, NECTA imemfutia matokeo mtahiniwa mmoja aliyebainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo. Mwaka jana watahiniwa 13 walifutiwa matokeo yao kwa kufanya udanganyifu.
Hata hivyo, Baraza hilo limesita kutoa matokeo ya shule zilizofanya vibaya kwa madai ya kuendelea na uchambuzi wa kuzitambua zaidi.