KINSHASA, DR
KAMPENI za uchaguzi wa urais nchini hapa zimeanza jana huku wasiwasi ukitawala baada ya wafuasi wa Rais Joseph Kabila kuchinjwa huku upinzani ukiwa umegawanyika.
Mwishoni mwa wiki iliyopita wafuasi watatu wa Chama tawala cha Rais Kabila waliripotiwa kuchinjwa katika jimbo la Kasai walipokuwa wakifanya kampeni.
Uchaguzi wa kumchagua mrithi wa Kabila aliyekaa madarakani kwa miaka 17 utafanyika Desemba 23, 2018.
Wiki iliyopita Martin Fayulu alichaguliwa kusimama kama mgombea kinara wa upinzani na ameungwa mkono na wapinzani wengine wenye ufuasi mkubwa kama Moise Katumbi na Jean Pierre Bemba.
Hata hivyo, chama cha upinzani chenye wafuasi wengi zaidi, Union for Democracy and Social Progress tayari kimejitenga na mgombea huyo.
Chama hicho kinachoongozwa na Felix Tshisekedi kimekuwa mstari wa mbele kuupinga utawala wa Kabila.
Kiongozi mwingine wa upinzani, Vital Kamerhe pia alijitoa kwenye makubaliano hayo akisema hakukuwa na uungwaji mkono wa kutosha kwenye mashina miongoni mwa wanachama.
Endapo mgogoro huo ndani ya upinzani utaendelea kupamba moto itakuwa ahueni kwa mgombea kutoka chama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary.
Shadary anaonekana na wengi kuwa ni kibaraka wa Kabila ambaye amezidisha muda wake madarakani kwa miaka miwili.
Siasa za DRC zimekuwa zikitawaliwa kwa mkono wa chuma na Kabila ambaye chini yake vyombo vya usalama vilitumika kuudhibiti upinzani kwa nguvu kubwa.
Mapema mwezi huu wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Kinshasa waliuawa kutokana na majeraha ya risasi walizopigwa na polisi wakati wa maandamano ya amani.
Polisi hao walichukuliwa hatua huku wakubwa wao, ambao ndiyo waliotoa amri ya kuvamia chuo hicho wakiachwa.
Agosti mwaka huu, watu wengine watano waliuawa katika maandamano mjini Lubumbashi walipoingia mtaani kwa maandamano ya kupinga kuzuiwa kwa Katumbi kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa uchaguzi huo kukumbwa na vurugu kutokana na chuki za siasa na uhasama baina ya raia na vyombo vya usalama.