26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kampeni chafu urais CCM zapamba moto

KinanaJOTO la uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), linazidi kupamba moto, huku uongozi wa juu wa chama hicho ukihaha kuwazima makada wanaodaiwa kuanza kampeni kabla ya muda.
Kutokana na hali hiyo, CCM imewataka wapambe na wagombea wao kuacha kutoa taarifa za uzushi dhidi ya makada sita wa chama hicho kwa lengo la kupotosha umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana visiwani Zanzibar, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema chama hicho kitawachukulia hatua kali makada wanaotaka urais na wapambe wao watakaobainika kusambaza taarifa za uzushi.
Pamoja na hali hiyo, CCM imewataka wagombea hao kuwadhibiti wapambe wao na kwamba wajichunge wenyewe dhidi ya hujuma kwa chama kwani zinaweza kuwapotezea sifa za kugombea.
Alisema pamoja na chama kutoa tahadhari kwa baadhi ya makada wake wanaotaka kugombea urais, lakini bado wameendelea na harakati hizo.
“Pamoja na kutotolewa kwa ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama, bado zimekuwapo harakati nyingi za wanaotaka kuteuliwa na CCM kugombea nafasi mbalimbali, hasa ya urais, ambapo baadhi ni halali, na nyingi haramu.
“CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaosambaza taarifa hizi. Ni vema wagombea wakawadhibiti wapambe wao na wakajichunga wenyewe dhidi ya hujuma hizi kwa chama kwani zitawapotezea sifa za kugombea,” alisema Nape.
Alisema kikao cha Kamati Kuu kilichoketi mjini Unguja Januari 13, mwaka huu, kilipitisha ratiba ya shughuli za kawaida za chama kwa mwaka 2015, huku ikipanga kushughulikia ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM vikao vijavyo.
Nape alisema pamoja na kutotolewa kwa ratiba hiyo bado zilikuwapo harakati nyingi za wanaotaka kuteuliwa na CCM kugombea nafasi mbalimbali, hususan za urais.
“Kwa muda sasa kumekuwapo na uzushi mwingi juu ya baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo kujadiliwa na hata kuchukuliwa hatua na vikao vya chama. Maneno haya kwa sehemu kubwa yamekuwa yakisambazwa na wagombea wenyewe au wapambe wao.
“Uzushi huu hauna nia njema kwa CCM, una lengo la kukigawa chama na kuonyesha kama vile hakina kazi nyingine ila kujadili na kushughulika na watu hao,” alisema Nape.
Hata hivyo, aliwatahadharisha wagombea na wapambe wao kujiepusha na kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli kwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kukigawa chama.
Aidha alisema wengi wanaosambaza taarifa hizo ni wagombea au wapambe wasiojiamini kutokana na matendo yao ambayo wana shaka na uadilifu wao.
“Hatuoni sababu ya mgombea anayefuata sheria, kanuni na taratibu za chama kuhofia kuchukuliwa hatua kila vikao vya chama vinapofanyika. Ukitenda kwa haki huna haja ya kuogopa vikao na kuzusha uongo na uzushi usio na ukweli. CCM inaamini matendo haya hayatajirudia,” alisema Nape.
Alisema Kamati Kuu iliitaka Kamati Ndogo ya Maadili kukaa na kushughulikia masuala ya kimaadili kuhusu makada wake waliopata mgawo wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Kwa mujibu wa taratibu, taarifa za kilichotokea kwenye kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili huwa hazitolewi kwa umma hadi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu. “Hivyo basi, tunawaomba kutulia na kusubiri taarifa rasmi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu,” alisema Nape.
Wakati taarifa hiyo ya Nape inakuja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba juzi alikuwa na ziara katika mikoa kadhaa huku akiwa ameambatana na baadhi ya wenyeviti wa mikoa.
Katika ziara hizo, Mwigulu alikuwa akitumia chopa inayomilikiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Kasheku Musukuma hali iliyotafsiriwa kama mikakati yake ya kujiimarisha na mbio za kuwania uteuzi wa chama hicho za urais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles