26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati yaundwa kuchunguza viungo vya binadamu

mabaki ya miili ya watu
Wananchi wakiangalia mifuko yenye viungo mbalimbali vya binadamu vilivyokutwa katika Bonde la Mweni Mpiji wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Picha ndogo kushoto ni polisi wakipakia viungo hivyo. Picha zote na Deus Mhagale

Adam Malinda na Grace Shitundu, Dar es Salaam

SERIKALI imeunda kamati ya watu 15 kuchunguza chanzo cha tukio lililofanywa na Chuo cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) la kutupwa mabaki ya viungo vya miili ya binadamu katika bonde la Mto Mpiji, lililopo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kuunda kamati hiyo imekuja siku chache baada ya kuthibitishwa kuwa mabaki ya miili iliyotupwa ilitoka Chuo cha IMTU.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema kamati hiyo itakayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaundwa na wataalamu kutoka taasisi sita tofauti.

Alisema kamati hiyo inatakiwa kukamilisha kazi yake kwa muda wa siku saba kuanzia Julai 23, mwaka huu na baada ya majibu ya kamati, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watu wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.

“Tumeunda kamati ambayo itakuwa na wataalamu kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Chuo cha IMTU ili kujua chanzo na watu waliosababisha tukio hili.

“Tumefanya hivyo kwa sababu tumeona kuna kosa limefanyika, kwani tukio hili ni la kwanza kutokea Tanzania tangu tulivyoanza kutoa mafunzo ya udaktari katika vyuo vyetu zaidi ya miaka 40 iliyopita,” alisema Dk. Kebwe.

Alisema miaka yote vyuo vimekuwa vikifanya mafunzo kwa kutumia miili ya binadamu na halikuwahi kutokea tukio la uvunjaji wa heshima ya miili hiyo.

“Vyuo vikuu vyote vinavyotoa mafunzo ya tiba vinaongozwa na sheria ya mwaka 1963, ambayo inaruhusu matumizi haya duniani kote na inaainisha taratibu za kuipata, kuisafirisha, kuihifadhi, kutumia na kusitiri mabaki baada ya matumizi,” alisema.

Alisema kuisitiri miili hiyo kunafanyika kwa kufuata sheria, maadili, utamaduni na miiko ya jamii husika, kuzingatia afya ya jamii na heshima kwa utu wa binadamu.

Alisema utaratibu wa kuhifadhi mabaki ya miili hiyo unajulikana kwa vyuo vyote ambao ni kuichoma hadi kuwa majivu au kuizika kwa taratibu za kawaida zinazofanywa za kuzika mwili wa marehemu.

Katika hatua nyingine, Dk. Kebwe alikitaka Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kuwashughulikia madaktari wote ambao watagundulika kuhusika katika tukio hilo.

“Katika kamati kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atashughulika moja kwa moja na uvunjifu wa sheria, lakini tunawataka MAT kumshughulikia daktari yeyote atakayebainika kukiuka sheria na maadili ya kidaktari, kwani madaktari wote huwa wanakula kiapo cha kuwa na maadili katika kazi yao,” alisema Dk. Kebwe.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha IMTU, imepinga vikali kauli ya Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Primus Saidia ya kutaka chuo hicho kifutwe.

Rais wa jumuiya hiyo, Meekson Mambo aliliambia MTANZANIA kuwa Rais wa MAT alikurupuka bila kujali mustakabali wa maamuzi anayotaka yachukuliwe kwani kufanya hivyo ni kutaka kuwahukumu watu wengine wasiohusika kwenye tukio hilo.

“Tumesikitishwa na kauli aliyoitoa Rais wa MAT katika vyombo vya habari bila kufika chuoni na kupata uhalisia wa sura ya tatizo kupitia Serikali ya wanafunzi,” alisema Mambo.

Alifafanua kuwa alichotakiwa kufanya Dk. Saidia ni kusikiliza maoni ya wanafunzi juu ya tukio hilo sanjari na kuwaona viongozi na mmiliki wa chuo kupata ukweli kwa kuwa uamuzi wa kukifuta chuo una athari kubwa kwa wanafunzi wenyewe na jamii kwa ujumla kwa kuwa adhabu hiyo haisaidii kuondoa tatizo lililojitokeza.

Naye Makamu wa Rais, Walter Nnko, alielezea kusikitishwa na mitazamo ya jamii kwa kuwazomea wapitapo mitaani na kuiasa jamii kuelewa kuwa wanafunzi wa chuo hicho hawahusiki na upatikanaji wa miili hiyo.

“Nahisi jamii haifahamu ukweli, kupitia taarifa yetu hii tunaomba ijue wanafunzi hatuhusiki kwa namna yoyote na upatikanaji wa miili ya wafu hao katika mazoezi ya vitendo, tunachofanya sisi si kigeni katika taaluma ya udaktari, ulimwenguni kote kinachofanyika ni kufanya mazoezi ya vitendo kwa wafu,” alisema Nnko.

Alisema kuwa anawashukuru viongozi wa dini, vyombo vya dola, taasisi za haki za binadamu na wananchi kwa ujumla kwa kusimama kidete kujua tatizo hili na kulikemea.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Serikali hiyo, Edward Mhina, alisema jumuiya yao inalaani kitendo cha utupaji wa miili hiyo kwa kuwa inakiuka maadili na sheria za mafunzo ya udaktari.

“Tanzania ina uhaba wa madaktari, MAT inashinikiza chuo hiki kifutwe, tunaelekea wapi tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake,” alisema.

Mabaki ya miili ya binadamu yaliyokuwa kwenye mifuko 85 ya plastiki ilikutwa Jumatatu wiki hii ikiwa imetelekezwa maeneo ya Mto Mpiji, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na haikujulikana mara moja imetoka wapi, kabla ya polisi kufanya uchunguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles