26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

KAMATI YAELEZA JINSI MAKONDA ALIVYOTISHIA WATANGAZAJI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

KAMATI ya muda iliyoundwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuchunguza tukio lililodaiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuvamia kituo cha utangazaji cha Clouds, jana imewasilisha ripoti yake.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imethibitisha kuwa ni kweli kiongozi huyo alivamia kituo hicho Machi 17, mwaka huu akiwa na askari waliokuwa na mitutu ya bunduki.

Akisoma ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa kamati hiyo, Deodatus Balile, alisema ni kweli Makonda alivamia ofisi hiyo, na kwamba alifika kwa gari yenye namba T 503 DFH.

“Baada ya kupewa kazi hii na Waziri Nape, tulikusanya taarifa za kilichotokea Machi 17,  ambapo Machi 19 ndiyo taarifa zilianza kusambaa.

“Katika uchunguzi wetu tulikuwa na hadidu za rejea tatu; kwanza kuthibitisha iwapo tukio lilitokea, pili kukusanya taarifa kutoka Clouds na Makonda na hatua za kuchukua kwa yeyote aliyebainika.

“Machi 20, mwaka huu kuanzia saa saba mchana hadi tatu usiku, tulifanya mahojiano na wafanyakazi 14 wa Clouds, wakiwamo wale waliokuwa kazini na kuangalia picha za ulinzi za CCTV kamera ambazo zimesambaa na tuliifanya kuanzia saa tatu hadi nne usiku,” alisema Balile ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Alisema baadaye walifanya juhudi za kumtafuta Makonda ikiwa pamoja na kumpigia simu.

“Pamoja na kwamba tulimpigia simu ya kutaka kuonana naye hakupokea, tukampelekea ujumbe hakujibu, tulitumia wasaidizi wake na Machi 21, saa 5:11 asubuhi hadi saa 6 mchana tulielezwa kuwa yupo ofisini na Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene na Saa 6.30 tukaelekezwa tuingie ndani kupitia mlango wa mbele.

“Wakati tunaambiwa tuingie kwa mlango wa mbele, kumbe Makonda alipitia mlango wa nyuma, Katibu wa RC akaja akasema tusubiri anakwenda pale Machinga Complex, tulikaa pale mpaka saa 9:00 mchana baadaye tukaambiwa tena kuwa amepata shughuli nyingine,” alisema Balile.

Kutokana na hilo, alisema kamati imejiridhisha pasipo na shaka kwamba Makonda hakutaka kutumia fursa kuwasikiliza.

Balile alisema chanzo cha hayo ni habari iliyokuwa itangazwe na kipindi cha Shilawadu inayomhusu Grace Athumani, anayedaiwa kuzaa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Alisema baadaye Makonda alikwenda kushinikiza kipindi hicho kitoke bila kukosa na hata pale alipoelezwa kuwa kipindi hakijakamilika, aliendelea kushinikiza.

“Tulijiuliza katika uvamizi huo, aliingia mpaka studio na askari aliokuwa nao, aliingia mpaka maeneo ambayo hawakupaswa kuingia bila idhini.

“Askari hao waliingia mpaka studio inayorusha matangazo mubashara na kamati imebaini kuwa kulikuwa na vitisho, askari kuingia wakiwa wameshika silaha za kibabe na Makonda aliwatisha kuwa angewafunga ndani ya miezi sita kama hawatarusha habari yake,” alisema.

Kwa mujibu wa Balile, mkuu huyo wa mkoa aliendelea kutoa vitisho kuwa angeweza kuwafunga watangazaji wa kipindi hicho kuwa wanajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.

Alisema vijana hao baada ya kupata vitisho hivyo, walipata taharuki na kwamba hata kipindi hicho hakikufungwa siku hiyo.

Balile alisema Makonda aliishikilia Clouds kwa muda wa saa moja, huku akiwaambia watangazaji hao kuwa yaliyotokea yabaki humo humo ndani na endapo watayatoa nje watamtambua yeye ni nani.

Alisema kamati pia imebaini kuwa kulikuwa na viashiria vya kuingilia uhuru wa uhariri kutokana na vitisho hivyo.

“Makonda alijipa jukumu la kiuhariri kwa kuhoji aliyezuia habari yake,” alisema.

Balile alisema kitendo cha Makonda kulazimisha habari ambayo haijahusisha pande zote irushwe, alikuwa amekiuka sheria za nchi.

“Azimio la Dar es Salaam kifungu 23, Serikali inapaswa kuondokana na ubabe kama kutumia vitisho, kuharibu vitendea kazi, uchunguzi makini ufanyike na wahusika washughulikiwe.

“Sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta, inazuia kurusha habari ambayo imeegemea upande mmoja,” alisema Balile.

Pamoja na hilo, alisema kamati imejiridhisha kuwa Makonda alikuwa mgeni mwenyeji na kwamba Machi 14, mwaka huu, alikaa katika ofisi za Clouds hadi Saa 10 alfajiri akiandaa kipindi cha mwaka mmoja.

Balile alisema wafanyakazi wa Clouds walishangazwa kwa kitendo hicho cha mkuu wa mkoa kufika na askari wenye bunduki na kwamba hawakuwahi kushuhudia askari wakiingia hapo studio.

Alisema pamoja na taarifa ambayo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa askari hao waliwapiga wafanyakazi hao, lakini kamati imebaini kuwa hakukuwa na vithibitisho vyovyote tofauti na kilichoonekana katika vyombo vya habari na mitandao.

MAONI

Balile alisema kamati imebaini Makonda alichokifanya kina viashiria vya uvunjifu wa sheria na dalili za kutotambua ukuu na madaraka aliyonayo.

Pia kamati hiyo iliupongeza uongozi wa Clouds kwa kusimamia misingi ya habari.

MAPENDEKEZO

Balile alisema Makonda anatakiwa kuwaomba radhi wafanyakazi wa Clouds na vyombo vya habari nchini.

Pia kamati hiyo ilimtaka Nape kusimamia na kulinda masilahi ya wanahabari na kwamba awasilishe mapendekezo hayo kwa mamlaka yake ya uteuzi na kuchukua hatua stahiki.

Kamati hiyo pia ilivitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kuwabaini askari waliotumika ili jambo kama hilo lisijirudie baadaye.

Balile alisema kamati imeitaka Clouds kupitia upya miongozo, kanuni na taratibu mpya za kuzuia watu wasiohusika kuingia katika chumba cha habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles