Na Zuena Msuya, Pwani
Kamati ya Uwezeshaji ya Mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi huo.
Mmoja wa wajumbe Kamati hiyo Albert Chile, akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, amesema kuwa wamefanya ziara hiyo Juni 23 na 24, 2021, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi wa mradi husika na hatua iliyofikiwa kulingana na makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani.
Chile alisema kuwa, kamati imekuwa ikifuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo tangu hatua za awali hadi sasa, ambapo pamoja na mambo mengine, baada ziara hiyo, imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na wanaimani kuwa utakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Alieleza kuwa kamati hiyo imeundwa mahsusi ikihusisha wajumbe kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali kwa lengo la kurahisisha na kufuatilia utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha majukumu yote katika makubaliano ya mkataba yanatekelezwa kwa wakati sahihi pamoja na kuishauri serikali.
Kamati hiyo ilitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa Mradi huo ambayo ni Handaki la Kuchepusha Maji ya Mto, Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, Kituo cha Kuchochea Umeme pamoja na Nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme.
Aidha walitembelea na kukagua Daraja la Kudumu, Barabara, Njia ya kupitisha maji ya kuzalisha umeme, pamoja na eneo la ufungaji wa mitambo.
“Tumetembelea, tumekagua na tumeona maendeleo ya mradi, kasi ya ujenzi inaendelea vizuri kuna mabadiliko makubwa sana ukilinganisha na huko nyuma, tunaimani ya kwamba Mkandarasi atamaliza kwa muda uliopangwa, hakika mradi huu ni ndoto ya Serikali na watanzania kwa jumla ya kuzalisha umeme mwingi zaidi hapa nchini kupitia vyanzo mbalimbali, ili kuwa na umeme mwingi wa bei nafuu na wa uhakika kwa watumiaji,” alisema Chile
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Christopher Bitesigirwe, alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022 na kwamba mkandarasi amelipwa zaidi ya Sh trilioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 100 ya malipo ya kazi iliyofanyika katika mradi huo. Kuanzia Novemba, mwaka huu, maji yataanza kujazwa katika bwawa hilo.
Mhandisi Bitesigirwe, alisema kuwa kutokana na Serikali kuendelea kutimiza wajibu wake wa kulipa madai ya Mkandarasi kwa wakati katika kipindi cha miezi 24 bila kuchelewa, hadi kufika Desemba 2020, tangu kuanza kwa mradi huo, imefanikiwa kupata nyongeza ya asilimia moja zaidi katika fedha zitakazotolewa na mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Alifafanua kuwa asilimia moja ya Fedha hizo ni zaidi ya shilingi Bilioni 65 ambazo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na hivyo kufanya thamani ya gharama za miradi ya kijamii kufikia zaidi shilingi bilioni 262.
“Wakati wa majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo, ilikubalika kuwa endapo mkandarasi atalipwa madai ya kazi alizofanya kwa wakati bila kuchelewa madai ndani ya kipindi cha miezi 24, kiasi cha fedha za kwa miradi ya kijamii kitaongezwa kwa asilimia 1 ya gharama za mradi, hivyo serikali imetekeleza wajibu wake kimkataba na kufanikiwa kupata nyongeza ya fedha hizo,” alisisitiza Mhandisi Bitesigirwe.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bitesigirwe,utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa JNHPP kwa ujumla umefikia hatua nzuri, huku kazi za ujenzi zikiendelea kwa lengo la kuzalisha Megawati 2115 za umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji.
Baada ya wajumbe hao kutembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, walifanya kikao cha pamoja na wameishauri serikali kupitia wizara na taasisi husika kutilia mkazo suala la kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kuweza kupata mvua za kutosheleza uwepo wa maji katika mradi wa JNHPP.