Na Fredy Azzah, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, imemshauri Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kufanya jitihada za kusuluhisha migogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa amesema hayo bungeni leo Jumatano aprili 4, wakati akitoa maoni ya kamati yake kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, mwaka 2018/19.
“Kamati inashauri Ofisi ya Msajili kuchukua hatua hizo kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano,” amesema.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kamati iliitaka tume hiyo kuendelea kuboresha daftari la wapigakura na kuchukua jitihada za kutosha katika kuboresha daftari hilo.
“Hatua hizo zijumuishe utoaji elimu ya uraia hususani uandikishaji wa wapiga kura kwa vijana waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga au kupigiwa kura.
“Tume inapaswa kujitahidi kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kuaminika kwa wadau wa uchaguzi kwa kuhakikisha inawashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa uhuishaji wa daftari la wapigakura kuepuka migogoro isiyokuwa na tija kwa taifa.
“Kamati inashauri tume ihakikishe inawafuatilia wasimamizi wake wa uchaguzi na kuwawajibisha pale wanapofanya uzembe unaosababisha madhara yanayoweza kudhibitiwa,” amesema.