Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka Serikali kuwezesha Wakala Majengo Nchi (TBA) ili kuendelea kutatua changamoto ya makazi kwa wakaazi mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo Machi 20,2024 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti na PIC, Deus Sangu wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Magomeni Kota awamu ya pili.
“Katika kikao chetu na Menejimenti ya TBA tumepata fursa ya kuoneshwa mpango wa ujenzi wa majengo ya makazi katika eneo hili la Magomeni Kota ambapo tumeshuhudia jengo moja limekamilika na jengo la pili likiwa limefikia 96%,” amesema Sangu.
Vile vile amepongeza uwekezaji huo uliofanywa na TBA kuwa unakwenda kutatua changamoto ya makazi kwa wakaazi wa jiji la Dar es Salaam kwa kupata makazi ya uhakika.
Pia ameitaka Serikali kuhakikisha inatoa fedha kwa wakati ili kukamilisha mpango huo wa ujenzi wa majengo matano katika eneo hilo kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa makazi kama ilivyokusudiwa kwa kuwa TBA imefanya uwekezaji wenye tija.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuruhusu kufanyika uwekezaji ambao unagusa wananchi wa hali zote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA Arch. Dk. Ombeni Swai, ameishukuru kamati kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuendelea kuisimamia Menejimenti ya TBA katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.