Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wa Kariakoo, Dar es Salaam, wamelalamikia baadhi ya askari na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanaowakamata wateja wao raia wa nje na mikoani kwa kosa la kutotambua bei za bidhaa zilizoandikwa kwenye risiti zao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Abdallah Mwinyi, alisema hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wateja wao na kuwafanya wahamie katika masoko mengine ndani na nje ya nchi.
Alisema kwamba kuwakamata huko kunawaongezea gharama za kuishi Dar es Salaam kutokana na kuwachelewesha kwa madai ya kufanya ufuatiliaji katika maduka waliyonunulia bidhaa ili kujiridhisha kama bei zilizo katika risiti ni sawa na zilizopo dukani.
“Wengine wanawashikilia hadi siku tatu na baadaye TRA wanasema bei iliyoandikwa iko sawa, huku ni kumpotezea muda na kumwongezea gharama za kuishi akiwa hapa,” alisema Mwinyi.
Aliitaka Serikali ishughulike na wafanyabiashara wanaotoa risiti na si kuwasumbua wateja ambao huwa na muda mfupi wa kukaa Dar es Salaam.
“Tulipanga kufanya biashara hadi usiku ili kuwapunguzia wateja wetu siku za kukaa hapa, lakini utaratibu wa kumzungusha mteja kila duka alilonunulia bidhaa ili kuthibitisha bei ya bidhaa ni kuzidi kumchelewesha,” alisema Mwinyi.
Naye mfanyabiashara wa nguo, Grace Mosses, alisema utitiri wa kodi za Serikali Kuu na Jiji la Dar es Salaam, ndizo zinazosababisha bidhaa kupanda bei.
“Kariakoo ilikuwa kama Dubai kwa wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali, lakini kupanda kwa bei za bidhaa kutokana na kodi nyingi pamoja na kamatakamata inayoendelea hivi sasa, inawavunja moyo wateja wetu,” alisema Grace.
Aliongeza kuwa mashine za kielektroniki za EFD’s zilizotangazwa zinatolewa bure kwa wafanyabishara wenye mitaji iliyo chini ya Sh milioni 14, hazijatolewa.
“Hata sisi wenye vigoli (maduka madogo) tukienda TRA kuomba mashine hizo, wanataka tuzinunue kwa shilingi 600,000 wakati mitaji yetu haijafikia kiwango cha kununua.
“Kwahiyo, tunaomba mashine hizo zigawiwe bure kama ilivyoagizwa na Serikali,” alisema Grace.