Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa, ICC Alhamisi imemhukumu Dominic Ongwen, raia wa Uganda, ambaye zamani alikuwa kamanda wa kundi maarufu la waasi la Lord Resistance Army (LRA), kifungo cha miaka 25 jela, kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Dominic Ongwen, mwenye umri wa miaka 45, alipatikana na hatia mwezi Februari 2021, kwa mashtaka 61, yakiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na utumwa wa kijinsia, mwanzoni mwa miaka ya 2000, chini ya LRA, wakati huo likiongozwa na Joseph Kony, ambaye alitoweka, na hajulikani aliko.
Upande wa utetezi ulikuwa umeomba apewe kifungo cha miaka 10 kwa tuhuma za kutekeleza mashambulio ya wanajeshi wake kwenye kambi za wakimbizi kaskazini mwa Uganda.
Waathiriwa wa uhalifu wake walikuwa wameiomba mahakama kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.
“Niko mbele ya korti hii ya kimataifa na mashtaka mengi, na bado mimi ndiye mwathiriwa wa kwanza wa utekaji nyara wa watoto. Kilichonipata, siamini hata kilitokea kwa Yesu Kristo,” Ongwen alisema.
Kampeni yake ya kinyama ya kuanzisha serikali kulingana na amri kumi za Biblia ilisababisha zaidi ya watu 100,000 kufa na watoto 60,000 kutekwa nyara, mwishowe ikasambaa hadi Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Majaji walisema katika uamuzi wao wa mwezi Februari kwamba, Ongwen mwenyewe aliwaamuru wanajeshi wake kutekeleza mauaji ya zaidi ya raia 130 katika kambi za wakimbizi za Lukodi, Pajule, Odek, na Abok kati ya mwaka wa 2002 na 2005.