27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kakakuona aonekana Dar

Kakakuona
Kakakuona

Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

WAKAZI wa eneo la Sensera Pub, Mbezi Juu jijini Dar es Salaam wamefurika kumuona mnyama aina ya kakakuona ambaye alijitokeza juzi usiku.

Taarifa za kujitokeza kwa mnyama huyo zilisambaa hadi chumba cha habari cha gazeti hili ambalo lilifika eneo hilo na kushuhudia umati wa watu ukiwa nje ya nyumba ya Martha Boniface ambaye alikuwa amemfungia kwenye moja ya vyumba vyake vya biashara.

Martha ambaye alikuwa mtu wa kwanza kumuona mnyama huyo ambaye ni aghalabu kuonekana, akitumika kama mtabiri wa mambo makubwa yanayoweza kutokea katika taifa, alisema alikiona kiumbe hicho juzi saa tano usiku kikiwa kinapita kwa mwendo wa taratibu.

“Tulikuwa tumekaa na wenzangu kama watano hapa nje jana (juzi) usiku, mara mmoja wetu akasimama akasema jamani mdudu huyo, niliponyanyuka nikamuona kakakuona anatembea anakuja tulipokaa, tulimpisha akasimama, badae akajikunja, tukamnyanyua na kumuingiza kwenye boksi kumuhifadhi,” alisema Martha.

Alisema baada ya kumuingiza kwenye boksi, walimpeleka ndani ya chumba cha ‘stationary’ na baadae ndani ya boksi ili aweze kuzunguka.

“Usiku ule ule nilichukua maji, kisu, unga na fedha shilingi 10,000 nikamuwekea vyote kwa pamoja, maji alikunywa yote, na unga alikula wote, fedha aliisogelea akainusa, lakini kisu alikipita akakiruka, hakukigusa wala kukinusa,” alisema Martha.

Akielezea sababu ya kumfungia ndani ya chumba hicho, Martha alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo ili asiondoke.

“Na usiku ule ule kabla sijafunga nikamtandikia kiroba ili asipate baridi la sakafu, lakini asubuhi nilimkuta kalala chini,” alisema Martha.

Kulingana na imani zilizopo nchini, kitendo cha mnyama huyo kula na kugusa vitu hivyo vitatu kati ya vinne, baadhi wanatafsiri kuwa ni ishara ya nchi kuwa na amani, mavuno mazuri na mvua za kutosha.

Kwa upande wake, Martha anachukulia kitendo cha kumuona kakakuona kinatoa tafsiri ya neema na bahati ambayo ameshushiwa na Mungu kwani kiumbe huyo huonekana mara chache.

MTANZANIA Jumapili lilishuhudia baadhi ya wananchi waliofika katika eneo hilo kwa nia ya kukishuhudia kiumbe hicho wakishikwa na mshangao wakati Martha akijaribu kukibembeleza kijikunjue katika gamba lake analolitumia kujificha ili kiweze kuonekana vizuri.

“Mgeni naomba uamke uwasalimie wenyeji wako wamekuja kukuona, tunajua umekuja kwa nia nzuri, umetuletea baraka, lakini watu wanatamani kukuona, naomba ujifungue ili uwasalimie wenyeji wako,” alisikika akisema Martha wakati akijitahidi kukifanya kiumbe hicho kijikunjue.

Baada ya muda kakakuona alianza kufungua miguu yake yote na kisha mkia, na baadae akaanza kutembea akizunguka huku na huko ndani ya chumba hicho.

Aidha mmoja wa jirani wa eneo hilo, Syntyche Sanya, alisema kwa mara ya kwanza alimuona kakakuona katika eneo  hilo Jumatano asubuhi wakati anaenda kazini.

“Mimi nilimuona saa 11 alfajiri wakati naenda kazini, kwa sababu nilikuwa simjui sikumfuatilia kabisa, nikajua ni mnyama wa kawaida,” alisema Sanya.

Mume wa Martha, Boniface Machera, alisema amefurahishwa na ujio wa myama huo mtaani kwao, lakini kutokana na umuhimu wake, waliamua kumuhifadhi hadi watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii watakapokuja.

“Tumemuhifadhi kwa sababu akiondoka kuna mawili, anaweza akapotea au watu wakamkamata na kumtoa magamba,” alisema Machera.

Aidha baadhi ya vijana waliofika kumuona kakakuona, walitumia tukio hilo kufanya utani.

Mmoja wa vijana hao alisikika akisema: “Tumemuwekea bendera mbili, ya CCM na Chadema, lakini akaenda kuegemea ya Chadema,” alisema huku wenzake wakiangua kicheko.

Hata hivyo, alipoulizwa Boniface kuhusu taarifa hizo, alicheka na kusema kuwa walikuwa wanatania tu na hakuna bendera yoyote iliyowekwa.

Mara ya mwisho mnyama huyo alionekana  jijini Dar es Salaam Julai mwaka jana katika eneo la Buza na mwaka huu ni mara ya kwanza kujitokeza.

Alionekana pia Oktoba mwaka 2010 katika eneo la Bunju ambako wananchi walimuwekea nafaka, silaha za jadi, maji na vitu vingine, lakini alienda kuegemea panga akiashiria hatari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles