Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhan Kailima amesema kuna baadhi ya mambo Tanzania inapaswa kujifunza kutokana katika uchaguzi wa Kenya.
Pamoja na mambo mengine, amesema utaratibu waliotumia hauna tofauti na utaratibu uliotumika nchini katika uchaguzi mkuu uliopita lakini kuna baadhi ya mambo yanapaswa kuigwa kutoka kwao.
“Mfano matumizi makubwa ya teknolojia,utoaji wa elimu ya mpiga kura ambapo wao wameanza kipindi cha maandalizi ya kuboresha daftari la kupigia kura lakini sisi tutafanya kwa mwaka mzima, kufanya midahalo baina ya Tume na wananchi ili wapate nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa,”alisema Kailima.
Amesema tume hiyo ilifanya vizuri katika uchaguzi huu tofauti na tume zilizopita na kwa sasa wanachofanya ni kuhakiki matokeo kwenye fomu namba 34 A.
“Tume imefanya mambo mazuri sana na wamekuwa mfano hata kuna taasisi zimesema hivyo ikiwemo Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), hivyo nina kila sababu ya kumpongeza mtendaji mwenzangu,” alisema Kailima.
Aidha, ametoa wito kwa wanasiasa nchini kujenga utaratibu wa kuisifia Tume hata pale wanaposhindwa sio kusubiri mpaka washinde ndio wasifie.
Kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020, amesema NEC itafanya maboresho ya daftari la wapiga kura Januari 2018 ambalo alisema maandalizi yake yanaendelea vizuri kwa sasa.