29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kagame afunguka tena mgogoro na Tanzania

Paul Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda

KIGALI, Rwanda

BAADA ya mgogoro wa muda mrefu wa diplomasia kati ya Tanzania na Rwanda, Rais Paul Kagame, amesema nchi hizo mbili ni ndugu na yanayotokea yasingepaswa kutokea.

Kagame aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, akifafanua kuwa mataifa hayo yataendelea kuwa ndugu.

Akijibu swali la mwandishi mmoja kuhusu uhusiano wa nchi yake na Tanzania kwa sasa, Rais Kagame alisema hakuna sababu yoyote inayoweza kufuta au kuharibu uhusiano wa wananchi wa nchi hizo mbili jirani.

Kagame alisema matatizo yanayowakabili wananchi wa Rwanda yanafanana na yanayowakabili Watanzania kwa sababu wote ni Waafrika wenye changamoto sawa za maisha.

“Matatizo yanayowakabili Watanzania ni sawa na yale yanayowakabili Wanyarwanda… hawa ni ndugu zetu ni kaka zetu ni dada zetu, Waafrika wenzetu ambao tunachangia mengi,” alisema.

Alipoulizwa kama angezuru Tanzania kutokana na kuwapo msuguano wa diplomaisia baina ya nchi mbili hizo, Rais Kagame alisisitiza yote yanayotokea sasa yasingepaswa kutokea.

“Hii haipaswi kusubiri nifanye ziara au nisifanye ziara hiyo, ukweli unabaki palepale… sisi ni ndugu na ujumbe wangu ungekuwa hakupaswi kuwapo au kusingepaswa kutokea matatizo yoyote kati ya Rwanda na Tanzania,” alisema.

Rwanda na Tanzania zilikabiliwa na wakati mgumu kuanzia mwaka jana kutokana na kutofautiana mtazamo kuhusu jinsi ya kukabiliana na kundi la waasi wa Kihutu la FDLR linaloendesha mapambano dhidi ya Rwanda kutokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Baadhi ya mitandao ya nchi hiyo imemnukuu Rais Kagame akisema kuwa ni vema masilahi ya mataifa hayo pamoja na Afrika yakaangaliwa zaidi kuliko kutazama watu wenye muono wa karibu ambao lengo lao ni kusababisha matatizo.

Akizungumzia FDLR alisema baadhi ya watu wameamua kulifanya kuwa ni tatizo kubwa lakini ni kati ya vitu rahisi.

Tanzania na Rwanda ziliingia katika mgogoro wa diplomasia hadi kufikia hatua ya kutunishiana misuli baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzishauri Rwanda na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo DRC.

Ushauri huo ulipingwa vikali na Rwanda ikidai kwamba Rais Kikwete aliingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa kushauri wawe na mazungumzo na watu wanaoua raia wa nchi hiyo.

Katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari juzi, Kagame, aliviomba vyombo vya habari, wanasiasa na mitandao ya jamii kusaidia kuziba ufa wa uhusiano uliobomolewa.

Naye Rais Kikwete alipolihutubia taifa mwisho wa Juni mwaka jana alisema mgogoro baina ya Tanzania na Rwanda ulikuwa umemalizika rasmi.

Alisema hatua hiyo ilitokana na mazunguzo kati yake na Kagame yaliyofanyika Uganda.

Ingawa hakusema mgogoro huo ulimalizika vipi, Rais Kikwete alisema hatua ya mazungumzo baina yake na Kagame ndiyo chanzo cha mafanikio hayo yote.

Wakati hali ikionekana kutulia, Mei mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema uhusino wa Tanzania na Rwanda haukuwa mzuri.

Pamoja na mambo mengine, alisema lilikuwapo suala la watu kupenyeza maneno kati ya pande hizo mbili na kusababisha ziangaliane kwa jicho la shaka hasa kila mmoja anapomuana mwenzake akizungumza na adui yake.

Alisema pia kuwa waasi wa kundi la M23 walioondolewa DRC ni raia Rwanda.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kusema hadharani kuwa inao uhakika waasi hao ni raia wa Rwanda.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopeleka majeshi DRC ambayo kwa kushirikiana na yale ya Umoja wa Mataifa yaliwaondoa waasi hao DRC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles