27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAFULILA: UCHUMI UMEKWAMA TANGU MKAPA AONDOKE

 KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila
KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam


 

KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), David Kafulila, amesema uchumi wa Tanzania haujawahi kukua tangu enzi za utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyeuacha ukiwa asilimia 6.9.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam juzi usiku katika kipindi cha Mada Moto kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten.

Kafulila alisema ukuaji wa sasa wa uchumi ni asilimia saba ambao ni mkubwa kulingana na rekodi ya juu ya Afrika na duniani kupitia ripoti za kimataifa, lakini haujasogea huku masikini wakiongezeka.

“Ni kweli Serikali imejisifu kwa ukuaji wa uchumi wa asilimia saba, kiasi hicho ni miongoni mwa rekodi ya juu ya ukuaji Afrika na duniani kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kimataifa. Hata hivyo, ifahamike kwamba rekodi hii imekuwapo na imeendelea kuwapo tangu awamu ya Mkapa,” alisema.

Alisema hotuba ya mwisho ya Serikali ya Mkapa kwa bajeti ya mwaka 2005/2006 ilionyesha kuwa ukuaji wa uchumi ulikua kwa asilimia 6.9 na umeendelea kuwa hivyo miaka yote kwa asilimia sita hadi saba.

Pia alisema Mkapa alikabidhiwa nchi ikiwa katika hali mbaya ya uchumi, lakini alijitahidi kuuweka sawa.

“Mkapa alikabidhiwa nchi ikiwa na mazingira magumu ya kiuchumi, lakini aliacha misingi imara ya kiuchumi. Kwa mfano riba za benki alikuta ni zaidi ya asilimia 26, lakini aliacha zikiwa asilimia 14, akiba ya fedha za kigeni alikuta ya miezi miwili, akaacha ya miezi saba, Jakaya Kikwete (Rais mstaafu wa Awamu ya Nne) akabakiza ya miezi minne na itaendelea kuwa ya miezi minne kwa hali ilivyo. Mkapa alikabidhiwa nchi haikopesheki akaacha deni la Sh trilioni 10, JK ameacha zaidi ya deni la Sh trilioni 40 na linazidi kupaa,” alisema.

Kauli ya Kafulila imekuja siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kusema kuwa uchumi umekua kwa asilimia 7.2.

Dk. Mpango ambaye katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya mwishoni mwa mwaka jana alizungumzia hali ya uchumi wa taifa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana na matarajio ya hadi Juni, mwaka huu, alisema mwaka juzi uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 7.0 na mwaka jana kwa asilimia 7.2.

Wakati Dk. Mpango akiyasema hayo, Kafulila alisema tatizo kubwa la ukuaji huo ni kushindwa kupunguza idadi ya masikini wanaoongezeka kila mwaka.

“Katika uchumi kuna dhana mbili, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya uchumi. Ukuaji unapimwa kwa vigezo vya ongezeko la uzalishaji ndani ya mwaka katika nchi husika, bila kujali uzalishaji huo unahusisha watu wangapi, wenyeji kiasi gani. Unapimwa kwa vigezo kama kiasi cha uwekezaji, mfumko wa bei, mauzo nje, manunuzi nje, kiasi cha akiba (saving), matumizi ya Serikali na kadhalika,” alisema.

Kafulila alisema changamoto ya Serikali ya Kikwete iliyopaswa kushughulika nayo ilikuwa ni kufanya ukuaji wa uchumi na misingi yake aliyoiacha Mkapa ili itafsiri maendeleo ya uchumi kwa maana ya kuboresha maisha ya watu.

“Awamu ya nne ilishindwa jukumu hilo kwa kiasi kikubwa na awamu ya tano haionyeshi mwelekeo wa kupunguza masikini kwa kiasi kikubwa. Sababu ya uchumi kukua bila kupunguza masikini ni pamoja na sekta zinazokua kiuchumi kubeba watu wachache au kuwa na athari ndogo kwa watu wengi,” alisema.

Kafulila alisema hali ya mzunguko wa fedha katika uchumi ni mdogo na kwa kiasi fulani inatokana na Serikali kuziba mianya ya ‘dili’, lakini si msingi wa ukubwa wa tatizo.

Alisema sababu nyingine ni deni ambalo lina uwiano wa 80:20, kwamba asilimia 80 ni la nje na Serikali inalazimika kulipa wastani wa Sh bilioni 700 huku makusanyo ya ndani yakiwa ni Sh bilioni 1,100 na kwamba kwa mwaka huu Serikali imeongoza kwa kukopa Sh trilioni mbili  kuanzia Novemba, mwaka juzi hadi Desemba, mwaka jana.

“Miaka ya nyuma mikopo ya ndani kwa mwaka haikuwa inazidi shilingi trilioni moja na inakopa zaidi ndani kwa sababu imekwama mikopo ya Ulaya. Waziri wa Fedha alikiri kukosa mikopo nafuu na misaada toka Ulaya na kwamba wameamua kujielekeza nchi za Japan, China, Korea ya Kusini na India na sababu kubwa ni masharti ya siku zote kuwa Ulaya wanataka kuona demokrasia na utawala bora. Waziri anasema riba za Ulaya zimepanda toka asilimia sita hadi tisa bila kusema huko upande wa pili riba ni kiasi gani,” alisema.

Kafulila alisema kutokana na hilo makusanyo ya mwezi yanaishia kulipa deni na mishahara.

“Kama tunalipa Sh bilioni 700 na mishahara Sh bilioni 560, wakati makusanyo ni wastani wa Sh bilioni 1,100, unategemea nini? Ndiyo maana kwa mujibu wa ripoti za Benki Kuu (BoT) inaonekana wakati awamu ya kwanza inamaliza muda wake deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 1.7 na kwa miaka 10 ya Kikwete deni la ndani likafikia Sh trilioni 7.5 mwaka huu mmoja deni la ndani limefikia Sh trilioni 10 kwa maana ya nyongeza ya zaidi ya Sh trilioni 2,” alisema.

Alitoa suluhisho kuwa kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kuhakikisha kilimo kinainuka.

Katika hilo alisema tangu miaka ya 2000, tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Repoa zinaonyesha kwamba kilimo kikikuzwa japo kwa asilimia nane kwa miaka mitatu mfululizo kinaweza kupunguza idadi ya masikini kwa asilimia 50.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles