23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA: WALINIOMBEA NIFE HADI SASA NADUNDA

Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,Edward Lowassa(katikati), akiwa na mgombea udiwani wa Kata ya Mateves,Arumeru mkoani Arusha,Abel Jeremiah(anayepunga), wakiingia katika Uwanja wa Saccos jana kuzindua kampeni za uchaguzi mdogo katika kata hiyo.Kulia ni Meya wa Jiji la Arusha,Calist Lazaro.
Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,Edward Lowassa(katikati), akiwa na mgombea udiwani wa Kata ya Mateves,Arumeru mkoani Arusha,Abel Jeremiah(anayepunga), wakiingia katika Uwanja wa Saccos jana kuzindua kampeni za uchaguzi mdogo katika kata hiyo.Kulia ni Meya wa Jiji la Arusha,Calist Lazaro.

Na JANETH MUSHI – ARUSHA


 

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewataka  wapigakura wa Jimbo la Arusha Mjini kutovunjika moyo na kuwaeleza kuwa Mbunge wao Godbless Lema (Chadema) ambaye yuko mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo mjini hapa, atavuka salama katika kipindi kigumu anachopitia.

Alidai kuwa watu wenye roho mbaya wako wengi kwani hata yeye walimwombea kifo muda mrefu, lakini hadi sasa anadunda.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Mateves, Wilaya ya Arumeru mkoani hapa baada ya wananchi kupaza sauti wakimuuliza juu ya hali ya Lema.

Lema anashikiliwa katika gereza hilo kwa zaidi ya miezi miwili tangu alipokamatwa Novemba 2, mwaka jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kushtakiwa kwa uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Lowassa alisema kuwa alienda gerezani na Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, kumwona Lema ambaye alidai kuwa afya yake ni njema ila anasumbuliaa na jambo linalofanywa na Serikali ambalo hata wao hawalielewi.

“Tatizo nikisema maneno wanaandika sana kwenye magazeti, halafu wakubwa wanachukia, tulienda na Sumaye  kumwona Lema, ana afya nzuri ila anasumbuliwa na jambo linalofanywa na Serikali ambalo hatulielewi, siwezi kuzungumzia sana kwa kuwa suala hili liko mahakamani.

“Tunalielewa tatizo lake, tuko pamoja na Lema na wapigakura wake, tunamwombea Mungu amsaidie avuke salama, hawa watu wenye roho mbaya wako wengi, walisema nitakufa, lakini nadunda,” alisema Lowassa.

Akizungumzia uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 22, aliwataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Vijijini kusimamia kikamilifu uchaguzi huo ili mgombea wao Abel Jeremiah aweze kushinda.

Lowassa aliwahakikishia wananchi wa kata hiyo kushinda, kwani wamemsimamisha mgombea ambaye ataweza kusimama na kutatua kero zao zinazowakabili.

“Madiwani simamieni uchaguzi huu vizuri, ila mkilala mkanywa mbege tumekwenda na ninawakabidhi hapa kwa kiapo na ninawahakikishia tutashinda zaidi, ndiyo maana nimekuja kwenye uzinduzi wa kampeni hizi, nawaomba mumpe mgombea wa Chadema kura zote.

“Tunajenga hoja kwani kura zinapatikana kwa hoja, tukatae kuibiwa kura ndugu zangu kwani chama chetu kina nguvu sana, Mateves msilale bado mapambano, lindeni kura ili tushinde kwa kishindo,” alisema.

Lowassa alisema atahakikisha kuwa mgombea wao akishinda atatatua kero mbalimbali ikiwamo maji.

“Nawaahidi maji yasipokuja simameni barabarani mnizuie, nitakwenda nyumbani kwake kumtoa kwa mke wake ili atatue kero hiyo kubwa,” alisema Lowassa.

Awali akiomba kura kwa wananchi, Jeremiah aliahidi kusimamia mikopo kwa makundi ya akina mama na vijana kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Vijijini pamoja na kutatua kero ya maji.

Awali Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, aliwaagiza madiwani wa Chadema, Jimbo la Arumeru Magharibi kuhakikisha mgombea huyo anashinda vinginevyo wajiuzulu.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kuwa mahakama ilimvua udiwani mgombea wa CCM baada ya kuthibitisha kuwa alitoa taarifa za uongo kuhusu Abel, hivyo kuwaomba wananchi kutomchagua tena.

“Mahakama ilibaini kuwa madai ya Abel kudaiwa kuua siyo ya kweli, leo CCM wanaleta mgombea ambaye mahakama ilimuona ni muongo, uongo ni mbaya, akiwa kiongozi atasema yapi ya ukweli,” alisema na kuwataka wananchi kumchagua mgombea wa Chadema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles