Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Davidi Kafulila amesema kamwe hatosita kuvunja mikataba ya Wakandarasi wa ujenzi wa barabara mkoani humo, endapo watatekeleza miradi waliyopewa chini ya kiwango.
Kafulila ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 3, 2021 wakati wa zoezi la utiaji saini wa mikataba 19 ya ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Changarawe na mitaro kati ya Wakala wa barabara vijijini na mijini mkoa (TARURA) pamoja na Wakandarasi 16.
Amesema Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya barabara ndani ya mkoa wa Simiyu wanatakiwa waondokane na dhana ya kufanya kazi kwa mazoea huku akiwataka wakuu wa wilaya zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo iliyosainiwa.
“Niwatake wakandarasi wote mliopewa zabuni ndani mkoa huu, kama kiongozi wa mkoa huu sitosita kuvunja mkataba wa mkandarasi yoyote ambae atabaini amejenga chini ya kiwango.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na tabia ya Wakandarasi wengi ambao wamekuwa wakipewa kazi za ujenzi, lakini barabara nyingi zimejengwa chini ya kiwango ikiwemo mkandarasi ambaye alikuwa najenga barabara ya Matongo.
“Kuna huyo mkandarasi wa Matongo, nataka nipate maelezo kutoka kwa Meneja wa Tarura mkoa, kwani anaendelea na kazi ndani ya mkoa wakati barabara ile imemshinda licha ya kumtaka arudie lakini ameshindwa,” amesema Kafulila.
Katika hatua nyingine, Kafulila amesema kuwa kwa mara kwanza, wananchi wa mkoa wa Simiyu watashuhudia miradi 18 ya barabara ikitekelezwa kwa fedha zao wenyewe ambazo walikatwa kupitia tozo za mafuta.
Awali, akitoa taarifa Kaimu Meneja wa Tarura Mkoa Mathias Mugorozi amesema kwa mwaka wa fedha 2021/22 kiasi cha Sh Bilioni 18.2 zitatumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara.
Amesema kuwa kupitia fedha hizo na mikataba ambayo wamesaini, kila eneo la mkoa wa Simiyu kutakuwepo na kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ili kurahisha shughuli za maenedeleo kwa wananchi.
Amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo mwisho wa utekelezaji wake ni kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali 2012/22, ambapo alieleza ofisi yake imejipanga kuwasimamia ipasavyo wakandarasi wote ili wajenge miradi kwa kiwango kinachotakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi, Mhandisi Lameck Okech alisema kuwa watahakikisha wanatekeleza miradi waliyopewa kwa kiwango kilichobora huku akiomba malipo yao yafanyike kwa wakati.