Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Mkoa mpya wa Simiyu, David Kafulila amesema kuwa, atahakikisha anaendeleza yale yote mazuri hasa upande wa elimu ambayo yalianzishwa na mtangulizi wake ambaye alikuwa Mkuu wa mkoa huo sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.
Kafulila amesema hayo leo Jumanne Mei 15, 2021 wakati wa hafla ya kukabidhiwa ofisi, ambapo amesema kuwa kuteuliwa kwake kuwa mkuu wa mkoa huo siyo kwa ajili ua kuja kutengua bali kwa ajili ya kutimiliza.
Amesema kuwa Mkoa wa Simiyu umefanya vizuri katika sekta ya elimu chini ya Mtaka na kubainisha kuwa atahakikisha anaendeleza pale ambapo kiongozi huyo ameacha na kufika mbele zaidi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa, ameomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa mkoa huo, ili kuhakikisha wanafikia malengo makubwa ambayo mkoa umejiwekea na kuwaletea maendeleo wananchi.
“Mkoa wa Simiyu unazo raslimali nyingi kama mifugo, kilimo, madini jambo ambalo ni fursa kubwa kwa wananchi wa mkoa huu kuzitumia na kuweza kujiletea maendeleo,” amesema Kafulila.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akizungumza katika hafla ya kukabidhi ofisi amewashukuru watendaji wote wa serikali, viongozi, na wananchi kwa ushirikiano ambao walimpatia na kufikia malengo.