Na Derick Milton Simiyu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ameagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la kung’oa mazao ya wakulima kwenye mashamba yao ambao wamechanganya Pamba pamoja na mazao mengine.
Zoezi la kung’oa mazao hayo kwa wakulima lilikuwa likitekelezwa na Wakuu wa Wilaya kwenye mkoa huo, ambapo baadhi ya wakulikuwa waling’olewa kwa kushindwa kufuata kanuni za kilimo cha pamba ambazo zinakataka Pamba kuchanganya na mazao mengine.
Kafulila ametoa agizo hilo leo JUmatano Desemba 29, 2021 kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini Bariadi, ambapo ameeleza licha ya wakulima kuelimishwa kwa kiwango kikubwa bado kulikuwepo na baadhi ambao waliendelea kuchanganya.
Amesema wamegundua kuwa wakulima wameendelea kuchanganya na mazao mengine hasa mahindi, kutokana na kuwa na hofu ya kukumbwa na njaa kutokana na kuwepo kwa hatari ya ukame nchini.
Kafulila amefafanua zaidi kuwa wakulima ambao wamechanganya mazao yao na Pamba, waachwe kwa sasa ila msimu ujao wasisitizwe kufuata na kuzingatia kanuni na sheria za zao hilo.
Amesema kuwa mbali na elimu iliyotolewa kwa wakulima juu ya kutochanganya pamba na mazao mengine lakini bado kuna wilaya ambazo wakulima wake wameendelea kufanya hivyo kwa hofu ya kupatwa na njaa kwa msimu huu kutokana na uhaba wa mvua.
“Inaonesha Kampeni iliyofanywa na Balozi wa pamba na viongozi wa wilaya na mkoa ya namna bora ya kushiriki kilimo bora ilieleweka lakini baadhi ya maeneo imekuwa tofauti…na kutokana na mkoa wetu kutangazwa kuwa ni miongoni mwa mikoa itakayokabiliwa na uhaba wa mvua, wakulima wakaingiwa na hofu na kuamua kuchanganya mazao,” amesema Kafulila.
Amesema kwa kuzingatia yote hayo serikali ya mkoa imeona kuna haja ya kuwasamehe wakulima hao waliofanya hivyo kwa msimu huu wa mwaka 2021/2022 waachiwe lakini wakulima hao wachukuliwe idadi yao na msimu ujao waone kama watajirekebisha na kufanya vizuri.
Mbunge wa jimbo la Maswa mashariki, Stanslaus Nyongo, amesema anamshukuru mkuu wa mkoa kwa uamuzi wake wa kuwasamehe wakulima hao lakini maafisa ogani waendelee kuwaelimisha wakulima hao.
Ameongeza kuwa kitendo cha viongozi kungoa mazao ya wakulima ambao wamefanya hivyo kwa kujihami na janga la njaa ni kutengeneza chuki baina ya wakulima hao na serikali ingawa idadi ya waliofanya hivyo ichukuliwe ili isaidie kuwafuatilia kwa msimu ujao.
Sambamba na hilo amemsihi mkuu wa mkoa kufuta kesi 14 za wakulima waliofunguliwa kwa kosa la kuchanganya mazao hayo ili kuwapa fursa na muda wa kujutia na kujirekebisha.
Hata hivyo, alivyotafutwa Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga ambao ndiyo wasimamizi wa zao hilo, amesema kuwa hawezi kuzungumzia lolote kwenye maamuzi hayo.