Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ameagiza wazawa wa Malampaka wapewe kipaumbele kwenye ajira ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza/Isaka.
Maagizo hayo yametolewa mara baada ya mamia ya wananchi wa mji wa Malampaka Wilaya ya Maswa, kumuomba mkuu wa mkoa awasaidie kupata ajira kwenye kituo cha ujenzi wa SGR kutoka Mwanza kwenda Isaka kilichopo kwenye mji huo inayojengwa na kampuni ya CCECC ya nchini China.
Wananchi hao walitoa kilio chao katika mkutano wa hadhara uliondaliwa na Mkuu wa mkoa kusikiliza malalamiko yao kuhusu kubaguliwa katika masuala ya ajira pamoja na kudai kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwenye mradi huo.
Wamesema wakati mradi unatambulishwa kwa mara ya kwanza na viongozi wa serikali walielezwa kuwa wakazi wa eneo hilo ambapo panajengwa bandari ya nchi kavu watapewa kipaumbele kwenye ajira.
Wamesema kwa sasa shughuli zimeshaanza lakini waliopata ajira ni wachache ambao hawazidi 15 kulinganisha na idadi watu 300 walioko kwenye kambi hiyo ambapo wengi wametoka nje ya mkoa wa Simiyu.
“Mwanzoni tulielezwa mradi utakapoanza kipaumbele kitatolewa kwa wananchi ambao wanaishi katika eneo ambalo mradi unatekelezwa lakini cha kushangaza mambo yamekwenda kinyume wengi wa waajiriwa wanatoka nje ya mkoa wa Simiyu.
“Sisi tumekuwa tukibaguliwa katika masuala ya ajira na jambo baya zaidi katika kupata ajira hizo vitendo vya rushwa vimeshamiri, amesema mmoja wa wananchi Juma Lufuta.
Aidha wamesema licha ya kufuatilia na kutoa malalamiko yao kwa viongozi wa Shirika la Reli (TRC) walioko kwenye eneo hilo wamekuwa wakijibiwa kuwa hawana sifa jambo walilodai si kweli.
“Hata ajira ya kushika kibendera vya kuonyesha gari ipite au isipite kuna kazi inaendelea unakuta mtu anatolewa Dar es Salaam je, kwa mji wa Malampaka au mkoa mzima wa Simiyu hawapo watu wenye uwezo huo, napo panahitaji sifa ya namna gani?” alihoji Fatuma Said.
Kwa upande wake Naibu Meneja Mradi wa TRC, Mhandisi Alex Bunzu, amesema malalamiko ya ajira za upendeleo na baadhi ya wafanyakazi wa mkandarasi kuomba rushwa ili watoe ajira kwa wananchi yameshafanyiwa kazi.
“Malalamiko haya tumeshayafanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali, wafanyakazi waliohusika wameondolewa kwenye ajira na tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu tuhuma za rushwa na watakaobainika watachukuluwa hatua kali za kisheria,” amesema.
Kutokana na malalamiko hayo Kafulila ameagiza vyombo vya dola kufuatilia suala la rushwa kama lipo na wahusika watakaobainika kuchukuliwa hatua za kusheria.
Aidha ameagiza kupelekewa majina ya watu walioajiriwa kama wanatoka mkoa wa Simiyu au la kwani serikali imekuwa ikitaka wanufaika wa kwanza wawe wanaoishi eneo la mradi.