Na ELIYA MBONEA
-ARUSHA
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekabidhiwa rasmi Hospitali ya Jeshi Arusha yenye thamani ya Sh bilioni 5.6.
Hospitali hiyo ikiwa na vifaa vya kisasa imejengwa eneo la Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA), Monduli mkoani Arusha ambapo itachukua wagonjwa 50 wa kulazwa na 300 wa nje.
Akizungumza kwenye uzinduzi na makabidhiano Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi aliishukuru Serikali ya Ujeruman kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Alisema kuanza kutumika kwa Hospitali hiyo kutasaidia askari pamoja na wananchi kupata huduma za matibabu kwa ukaribu zaidi hususani waliopo jirani.
“Familia za wanajeshi na wananchi wanaozungumza maeneo haya watanufaika zaidi na ufadhili huu hii ni Hospitali ya kisasa kabisa yenye vifaa vipya na huduma zote,” alisema Waziri Dk. Mwinyi na kuongeza:
“Tunaendelea kuwashukuru Ujerumani kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili waweze kutumia vifaa hivi vya kisasa. Lakini pia wafadhili hawa wametujengea Chuo cha Tiba kilichopo Dar es Salaam,” alisema.
Alisema matumizi ya hospitali za Jeshi kwa wastani yamekuwa yakitumiwa kwa asilimia 20 huku asilimia 80 yakitumiwa na wananchi. Hivyo kutumika kwa Hospitali hiyo kutakuwa msaada mkubwa zaidi kwa wananchi.
“Wananchi waliokuwa wakisafiri kwenda Hospital za Rufaa wameletewa huduma hizo karibu. Serikali tutaendelea kushirikiana na wananchi katika huduma zinazotolewa ndani ya Jeshi ikiwamo masuala ya afya na mengine.
Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter aliyekabidhi majengo ya Hospitali hiyo na vifaa alisema, Serikali ya nchi yake itaendelea kusaidiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali.
Alisema miundombinu ya Hospitali hiyo iligharimu Sh bilioni 2.8 huku vifaa tiba vikigharimu Sh bilioni 2.8 ambapo fedha hizo zimetolewa na German Armed Force Technical Advisory Group (GAFTAG).
Naye Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo alisema Hospitali hiyo itakuwa ya Kanda kutokana na mkoa wa Arusha kutokuwa na hospital kubwa yenye uwezo wa kuhudumia askari.
“Arusha hapakuwa na Hospitali ya Kanda wanajeshi waliopo eneo hili ni wengi na Hospital zetu ni ndogo hazikujitosheleza kuwahudumia kwa wingi wao,” alisema Jeneral Mabeyo.
Aidha Mkuu wa Tawi la Tiba JWTZ Meja Jenerali Denis Janga alisema, Hospitali inatarajiwa kuanza kutoa huduma muda wowote baada ya kuzinduliwa na kukabidhiwa jeshini.
“Hospitali hii ina idara ya wagonjwa wa nje, wagonjwa wa ndani, dharura, mama na watoto, Radiolojia ikihusisha X Ray na Utrasound,” alisema Meja Jeneral Janga na kuongeza:
“Nyingine ni CTC, Maabara, Pharmacy, Mortuary, Karakana na sehemu ya kufulia,” alisema.