22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

 JPM: Walioua familia wakamatwe haraka  

1*Ataka wananchi wamwabudu Mungu maovu kama hayo yasitokee

Anna Luhasha na Judith Nyange, Sengerema

RAIS Dk. John Magufuli amesema amesikitishwa na mauaji ya kinyama ya watu saba wa familia moja waliokatwa mapanga katika Kijiji cha Sima wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwasaka kwa nguvu zote, watu waliohusika na mauaji hayo na kuhakikisha wanatiwa mbaroni ndani ya kipindi kifupi.

Akitoa salamu za pole nyumbani kwa wafiwa jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema Rais Magufuli ameguswa na tukio hilo na kusema umefika wakati wa wananchi kumwabudu Mungu ili maovu kama hayo yasitokee.

“Wakati nakuja huku, Rais Magufuli amenituma nimfikishie salamu zake za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki mliofiwa.

“Ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawasaka na kuwatia mbaroni watu waliohusika na tukio la kinyama ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Alisema Rais Magufuli ametaka wahusika wote wakamatwe ndani ya kipindi kifupi, kwa sababu mauaji ya aina hiyo hayakubaliki hata kidogo.

Samia alisema Rais Magufuli amewataka wananchi kumcha Mungu kwa kuwa wakishika imani na kumwabudu maovu yatapungua.

Alisema jamii ya wacha Mungu haina maovu mengi kama hayo.

Kuwasili kwa Samia katika msiba huo, kuliamsha vilio vingi kutoka kwa wananchi waliokuwapo.

Samia alitembelea sehemu ambayo ujenzi wa makaburi matano ulikuwa unaendelea kwa gharama za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.

 

MAZISHI

Miili ya watu hao watano inatarajia kuzikwa leo kijijini Sima.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sengerema, Yanga Makaga, alisema halmashauri inagharamia gharama zote za mazishi kama alivyoagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Alisema miili ya marehemu wawili itasafirishwa kwenda wilayani Ngara mkoani Kagera kwa mazishi kwa sababu walikuwa wafanyakazi wa mashamba.

“Jukumu letu tunagharamia usafiri, kuandaa majeneza na kuwasafirisha marehemu Samson na Donald ambao watazikwa Ngara. Tumekamilisha taratibu zote,” alismea Makaga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Julius Chalya, alisema shughuli ya utayarishaji wa majeneza na ujenzi wa makaburi kwa ajili ya kuhifadhi miili ya marehemu imekamilika.

Watu hao waliuawa kinyama kwa kukatwakatwa mapanga usiku wa manane, kuamkia Aprili 11, mwaka huu baada ya familia hiyo kuvamiwa na watu ambao idadi yao haijafahamika wakiwa wamelala katika nyumba tofauti.

Taarifa zilizopatikana wilayani Sengerema na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, zinasema mauaji hayo huenda yamefanywa na watu wawili au mmoja na chanzo chake hakijajulikana.

Mmoja wa wanafamilia, Patrick John akielezea tukio hilo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, aliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na Augenia Kutega (64), mama wa familia hiyo ambaye kabla ya kushambuliwa na mapanga hadi kupoteza uhai, alilazimishwa kutoa Sh 40,000.

Wengine ni Mariam Philipo ambaye ni mdogo wa Augenia, watoto Leonard Alloys na Leonard Thomas ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Sima, Donald na Samson ambao walikuwa wafanyakazi wa shambani.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alifika kijijini hapo akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kuagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika na ndani ya saa 48 wawe wamekamatwa wakiwa hai au marehemu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles