WAANDISHI WETU- DAR/ MOROGORO
RAIS Dk. John Magufuli amewatembelea majeruhi 43 wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), huku akiwataka Watanzania wasiwe wepesi kutoa hukumu.
Pamoja na hali hiyo amesema kati ya majeruhi hao wapo wengine waliokuwa safarini lakini walikumbwa na ajali hiyo wakiwa wanaendelea na safari, ambapo pia mewapatia kila kila mmoja Sh 500,000 kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Kutokana na ajali hiyo Rais Magufuli, ameagiza majeruhi hao wapatiwe matibabu ya daraja ya kwanza na serikali itagharamia matibabu hayo.
Hata hivyo, naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuongezeka kwa idadi ya vifo ambapo hadi jana jioni imefikia 71.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi Mtaa wa Itigi, Msamvu mkoani Morogoro ikiwa ni mita 200 kabla ya kufika kituo cha mabasi cha Msamvu baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi, ambapo watu walikuwa wameanza kuchota mafuta.
Kutokana na hali hiyo majeruhi 46 waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo watatu kati yao walifariki dunia jana.
Akiwa katika wodi za Sewahaji na Mwaisela, Rais Magufuli, alizungumza na majeruhi hao pamoja na kuwashukuru wauguzi pamoja na madaktari kwa huduma nzuri na kuwazawadia Sh milioni moja.
“Watanzania tuendelee kuwaombea ndugu zetu hapa walipo wameungua ndani na nje kama alivyoleza daktari hii ina maana wana majeraha ya moto lakini pia walikuwa wanavuta hewa ya mafuta ya petroli,” alisema Magufuli.
Mkuu huyo wa nchi aliwaagiza madaktari kuhudumia majeruhi hao pamoja na kuwapatia mahitaji yote wanayohitaji kwa gharama ya Serikali.
“Serikali italipa chochote watakachohitaji, wapatiwe matibabu daraja la kwanza endeleeni kuwahudumia na mumtangulize Mungu mbele lakini pia Watanzania kila mmoja katika imani yake waombeeni wenzetu wameumia sana wanapata mateso.
“Serikali itatoa matibabu yote ya wagonjwa chochote watakachokuwa wanadaiwa iwe chakula, maji , uji na matibabu nitalipa mimi na gharama zote niletewe mimi kwa niaba ya watanzania nitalipa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wapo majeruhi ambao walikuwa wanasafiri na wengine walikuwa wanawasaidia wenzao, hivyo sio wote waliopata ajali walikuwa wanachota mafuta .
“Niwaombe Watanzania tusiwe wepesi wa kuhukumu, kutoa hukumu ni kitu kibaya sana kwani kati ya majeruhi niliyowaona yupo dereva aliyekuwa akisafiri kutoka Tanga na alipoona ajali alishuka kusaidia naye ameungua.
“Ilikuwa ajali mbaya ambapo wengine wamepata taarifa kwamba wameungua kwa asilimia kati ya 80 hadi 100, jambo hili ni la bahati mbaya wengine walikuwa wanasafiri wakakumbana na tatizo,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli aliwata wataalamu wa afya hospitalini hapo kuhakikisha wanawahudumia wagonjwa hao kama taaluma zao zinavyowataka.
“Nawashukuru madaktari na wauguzi wanafanya kazi nzuri, natambua kazi mnayoifanya katika kuwahudumia majeruhi hawa hivyo nimekuja kuwaongezea nguvu,” alisema
Rais Magufuli aliwataka Watanzania kumtanguliza Mungu katika shughuli zao za kila siku ili waweze kuliokoa taifa.
“Tunapoomboleza tumtangulize Mungu na kuwaombea majeruhi hawa wapone haraka na kumwomba atuepushe na majanga na kulikoa Taifa letu,” alisema
MAJERUHI WASIMULIA
Mmoja wa majeruhi hao Rajabu Ally, ambaye alikabidhi kiasi cha fedha na Rais Magufuli, alimshukuru mkuu huyo wa nchini baada ya kuulizwa kuhusu ajali hiyo.
“Mimi nashukuru Mungu nimenusurika sikujua hata kilichotokea niliona tu moto unanifuata. Nilikuwa nasafiri kutoka Dodoma kwenda Mtwara trafiki alinisimamisha nikasimama ndipo ukatokea mlipuko huo na mimi kujeruhiwa hivi,” alisema Ally.
Naye majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha, ambaye ni mama lishe katika stendi ya mabasi ya Msamvu alimshukuru Rais Magufuli na kubainisha kuwa hakujua kilichotokea.
PROFESA MUSERU
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru alisema hadi sasa hospitali hiyo, imepokea majeruhi 46 ambapo watatu wameriki dunia.
Alisema majeruhi wengi wameungua kwa zaidi ya asilimia 80 na wataalamu wanafanya juhudi za kuokoa maisha yao.
TISA WALAZWA ICU
Aliongeza kuwa tisa kati ya wagonjwa hao wamelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), huku 33 wakilazwa katika wodi mbalimbali hospitalini hapo.
“Majeruhi 42 walifikishwa jana(juzi) usiku kwa kutumia magari ya wagonjwa ya dharura na wengine wanne wamesafirishwa kwa helikopta kutoka hospitali ya Mkoa ya Morogoro na kufika leo(jana),” alisema Prof Museru.
WATAALAMU 11 MORO
Alisema kuwa baada ya tukio hilo kutokea, hospitali hiyo ilituma wataalamu 11 kutoka vitengo mbalimbali kwenda kuongeza nguvu katika hospitali ya Morogoro.
“Tumeaandaa dawa za kutosha vikiwamo vitendanishi vyote vinavyohitajika kuhudumia majeruhi ambao wameanza kupatiwa matibabu,” alisema Profesa Museru.
HELKOPTA NA WAGONJWA
Jana majeruhi wengine wanne waliosafirishwa kwa helkopta walitua katika uwanja wa Jangwani saa 4:50 asubuhi na kuingizwa katika magari ya wagonjwa.
Safari ya kuwapeleka MNH ilianza huku askari wa usalama barabarani walitanda katika kila kona za barabara kuelekea Hospitali ya Taifa Muhimbili.
TUME YA UCHUNGUZI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameunda tume maalumu kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali ya moto, iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 71 hadi jioni ya jana na wengine kujeruhiwa wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka, mjini Morogoro.
Akizungumza jana mjini Morogoro na waombelezaji waliofika kutambua miili ya marehemu, ambapo Majaliwa alisema kuwa Waziri Mkuu ameunda tume hiyo ili kuweza kujua sababu za kina za ajali hiyo.
Alisema idadi ya vifo imeongezeka na kufikia wati 71 baada ya vifo vingine vitatu kutokea, ambapo wakati wa kusafirisha majeruhi kwenda MNH, mmoja wao alifariki njiani na kuongeza idadi ya waliofariki kufikia 69.
“Hata hivyo, majeruhi wengine wawili walifariki hapa Morogoro na hivyo takwimu kufikia vifo 71,” alisema Majaliwa.
Alitoa shukrani kwa watu wanaozidi kutoa michango mbalimbali ikiwamo dawa, damu na vifaa tiba.
“Niko mbele yenu nikimwakilisha Rais Dk. John Magufuli aliyenituma kuja kuungana nanyi kwenye siku hii ya huzuni. Hii tume inaanza kazi leo(jana), hadi Ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje.
“Ajali ya namna hii si mara ya kwanza ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi Watanzani pale gari linapoanguka tusitume kama fursa twende tukaokoe binadamu waliopo pale,” alisema Majaliwa.
Alisema ni lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake kwa sababu ajali imetokea saa mbili asubuhi katikati ya mji, hivyo wanataka kujua ajali ilipotokea kila mmoja kama alitimiza wajibu wake.
Waziri Mkuu alisema ajali hiyo imetokea karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi na kuna polisi lakini bado kuna maswali, kwamba sasa je hawa wananchi waliopata ajali walienda na madumu ya kuchotea mafuta ambapo waliamka asubuhi wakijua ajali itatokea?
“Najua pale ajali inapotokea trafiki wana wahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia.Je lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani.
“Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake. Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu. Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika kuwapoteza Watanzania,” alisema.
Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha kwamba zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona.
Akizungumzia kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo inatangazwa kupitia vyombo mbalimvali vya habari, Waziri Mkuu alisema ni vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Kebwe.
“Kwenye vyombo vya habari tuelewane katika takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini yake. Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyinginyingi mnajenga hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa mtafuteni mkuu wa mkoa,” alisema
Waziri Mkuu alisema wananchi wasipeleke miili kwanza makaburini ili waweze kupitia na kutambua ndugu na rafiki kwa ajili ya kuwa na kumbukumbu ya kudumu.
“Hali si nzuri ndugu zetu wameungua sana wapo wengine mnaweza msiwatambue lakini mnaweza kutambua kwa alama. Wapo wengine walivaa bangili, heleni, mkanda havijaungua,” alisema
WAZIRI JENISTA
Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama, alisema lita 166 za damu wananchi wamejitolea kusaidia kuokoa majeruhi waliopo hospitalini, na kwamba watu 48 wamejitokeza kubaini ndugu zao ambapo maiti 33 zimeshatambulika.
Aliongeza kuwa misaada mbalimbali imeendelea kutolewa Ikiwemo mablanketi , madawa, vifaa tiba na elimu ya saikolojia kwa waathirika wa tukio hilo.
Alisema tayari madaktari bingwa 10 kutoka hospitali za Mloganzila, Muhimbili na Benjamin Mkapa wameshawasili katika hospitali ya rufaa mkoani Morogoro kuendelea kutoa matibabu.
Ajali hiyo ilitokea Agosti juzi ambapo lori lenye namba za usajili T 717 DFF aina ya Scania ambalo lilikuwa na tela lenye namba T 645 CAN lililokuwa na shehena ya mafuta aina ya petroli na dizeli lililolipuka moto na kusababisha vifo.
UCHANGIAJI DAMU
Taasisi ya Suleimani Kova security Foundation(Sukos) walifika mapema kuchangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi hao ambao wanahitaji huduma ya kuongezewa damu kutokana na kuungua moto.
Akizungumza hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Sukos, Suleiman Kova, alisema ameshawishi watu 70 ambao ni wakimbiaji wa mwendo pole kwenda kutoa damu kwa ajili ya majeruhi hao.
“Niwaombe watanzania kuendelea kutoa damu kwa ajili ya wenzetu waliopata na changamoto hii kwa kuwa mahitaji ni makubwa lakini wachangiaji ni wachache,” alisema Kova.
Naye Mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia alifika akiwa na familia yake kutoa damu.
HABARI HII IMEANDALIWA NA na TUNU NASSOR, AVERINE KITOMARY (DAR), RAMADHAN LIBENANGA NA ASHURA KAZINJA (MOROGORO