25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM: Kuna walimu wanafanya ufisadi

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Asema wamekuwa wakisajili wanafunzi hewa

Na Mwandishi Wetu, Katoro

RAIS Dk. John Magufuli, amewaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa hadi kitongoji kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo, kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.

Agizo hilo alilitoa jana mkoani Geita, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Katoro  ambapo aliwaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa fedha za ruzuku (capitations) na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi yao.

“Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane.

“Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja naagizo hilo pia ametaka viongozi wa ngazi zote katika mikoa kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo.

Alisema kuanzia sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.

“Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tarafa, watendaji wa kata na wenyeviti wa vijiji kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi,” alisema

Kiongozi huyo wa nchi alitumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ikiwemo kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania mpya kwa kuwataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.

Licha ya hali hiyo Rais Magufuli, amekosoa utaratibu unaotumiwa na halmashauri nyingi za majiji, manispaa, miji na wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na kusema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika halmashauri husika.

“Hivi kwa nini halmashauri msingekuwa na maafisa wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya fedha?

“Tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma,” alisema na kuhoji Rais Magufuli

Rais Magufuli amehitimisha ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake Chato kwa mapumziko mafupi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles