ANDREW MSECHU– Dar es salaam
Rais JohnMagufuli amesema ameamua kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuhakikisha kuwa mali zote za Waislamu zilizochukuliwa isivyo halali zinarejeshwa.
Akizungumza katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) jijini Dar es Salaam leo Decemba 17, Rais Magufuli amesema alichukua uamuzi huo baada ya kupata ombi kutoka kwa Mufti, Sheikh Abubakar Zuberi ambaye alimweleza namna mali hizo zilivyochukuliwa na kumuomba asimamie zirejeshwe.
“Kwa jinsi Mufti alivyozungumza akupigania maslahi ya Waislamu, aliniambia kwamba awali nilipokuwa waziri nilishindwa kuzisimamia, lakini sasa mimi ni Rais na ninapewa mamlaka ya kisheria kupitia Katiba katika masuala ya ardhi.
“Aliniambia kwa kuwa wewe sasa ni Rais tusaidie hizi mali zirudi. Tena aliniambia akiwa amenikazia jicho, na kwa mcha Mungu unapoambiwa na kiongozi wa juu wa kidini kama Mufti ni kwamba umeambiwa na Mungu kwa hiyo ni lazima utekeleze,” amesema
Alisema baada ya ombi hilo la Mufti alimwita Waziri wa Ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa maagizo kwa viongozi wote aliowateua katika mikoa na wilaya akawataka waangalie namna ya kufuatilia mali hizo na kusaidia kuzirejesha, suala ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikiwa.
Rais Magufuli amesema katika mali ambazo zilikuwa na ugumu wa urejeshaji wake kutokana na mazingira na mikataba migumu aliamua kutumia mamlaka yake kuzifuta umiliki wake kutoka kwa waliokuwa wamejimilikisha au kumilikishwa.
“Niliwahi kufuatilikwa undani ni kwa namna gani mali za Waislamu zilichukuliwa au kupokonywa. Baada ya kufuatilia nilibaini waliohusika kuzigawa ni Waislamu wenyewe kwa kuingia katika mikataba migumu ambayo walishindwa kuisimamia na kuitekeleza,”alisema.