Na MWANDISHI WETU
DAR ES SALAAM
Rais Dk. John Magufu jana alirejea Dar es Salaam akitokea Zanzibar kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya hayati Baba waTaifa, Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika katika uwanja wa Amaan Mjini Magharibi.
Taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid, Amani Karume, Rais Magufuli aliagwa na viongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud.
Kabla ya kuondoka Ikulu Zanzibar, Rais Magufuli alikula chakula cha mchana na wakimbiza Mwenge mwaka huu walioongozwa na Amour Hamad Amour ambapo aliwahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa ya Mwenge waliyoiwasilisha kwake katika sherehe za jana.
“Mlipokuwa mkikimbiza Mwenge wa Uhuru nilikuwa nafuatilia miradi mliyokuwa mnatembelea na maelekezo mliyokuwa mkitoa, sehemu zote mlizobaini kuwepo kwa dosari ninawahakikishia kuwa tutazifuatilia na kuchukua hatua”alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema anatambua uzalendo waliouonesha wakati wote wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru na amewasihi kuendeleza maadili na uzalendo huo kwa manufaa ya taifa.