24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AMKAANGA MAKONDA

 

Na MWANDISHI WETU


RAIS John Magufuli amemkaanga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akishangaa kitendo chake cha kuyaingiza makontena 20 na kugoma kulipa kodi ya Sh bilioni 1.2.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli, inaweza kuhesabiwa kuwa ni msumari wa mwisho kwenye sakata hilo baada ya hivi karibuni mkuu huyo wa mkoa kushukiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Itakumbukwa kuwa wakati sakata hilo lilipoanza kupamba moto Mei mwaka huu, Makonda alisema endapo Mamlaka ya Mapato (TRA) na Dk. Mpango, wataendelea kushikilia makontena hayo bandarini, atawashtaki kwa Rais.

 

KAULI YA RAIS

Jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo, Rais Magufuli alisema viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa masilahi ya watu binafsi.

“Ni lazima sisi viongozi ‘no matter’ uko kwenye ‘position’ gani, tujenge mazingira ya kuwatumikia Watanzania, hizo ndizo sadaka zetu.

“Mmesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi kwanini asilipe? Kwa sababu katika sheria za nchi yetu ni mtu mmoja tu aliyepewa dhamana kwa mujibu wa sheria ambapo ni sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na misaada.

“Nafikiri kupitia sheria namba 30 ya mwaka 1974 kifungu cha 3, 6, 13 na 15, ndiye amepewa dhamana ya kupokea misaada kwa ajili ya nchi, hakuna mtu mwingine, hayupo.

“Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine au na wafanyabiashara, unasema una makontena yako, halafu unasema ya walimu wala hata shule hazitajwi.

“Hii maana yake nini? Si unataka utumie walimu ulete haya makontena, utapeleka shule mbili, tatu, ndizo zitapewa mengine utakwenda kuyauza kwenye ‘shopping mall’, lakini walimu walikwambia wanahitaji makochi? Wafanyakazi wasitumike kwa masilahi ya watu fulani,” alisema Rais Magufuli.

Mbali na hilo, aliwataka madiwani wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti, ikiwa ni pamoja na zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi.

 “Nafahamu kuwa hata ninyi madiwani huwa mnakaa kikao siku moja na mnataka kulipwa posho ya siku mbili au tatu au mtumishi wa halmashauri anasafiri kwa siku mbili, lakini anaandikiwa posho za siku nne.

“Nataka mchezo huu ukome, elekezeni fedha kwenye mahitaji muhimu ya wananchi, wakurugenzi na wakuu wa wilaya simamieni hilo,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, katika mkutano huo ambao alianza kwa kupokea maswali, kero na maoni ya wafanyakazi na viongozi, aliwahakikishia Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa kujitegemea na kutatua kero za wananchi.

“Mimi ni Rais wa Tanzania nzima si Rais wa Chato, nina wajibu wa kuhudumia Tanzania nzima, kwa hiyo mambo ya hapa Chato wabaneni viongozi wa hapa Chato,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu uhaba wa watumishi, alisema baada ya Serikali kuokoa Sh bilioni 138 zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi hewa na wenye vyeti feki, sasa imeanza kuajiri watumishi 52,000 na kwamba itaanza kulipa madeni ya watumishi baada ya uhakiki kukamilika.

 

ALICHOSEMA MAKONDA

Mei mwaka huu, Makonda alisema TRA na Wizara ya Fedha wanauhujumu Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba wakiendelea kuyazuia makontena hayo atawashtaki kwa Rais.
Alisema TRA wanakusanya kodi, halafu hiyo kodi ikishakusanywa inaenda kujenga shule na samani zikiwemo mbao za kufundishia.
“Sasa umepata mtu wa kukupa mbao za kufundishia zinazotumia umeme, walimu wetu wanateseka na chaki zinaingia puani, mtu analeta madawati, meza za walimu na vifaa vya kufundishia vya zaidi ya Sh bil 2, wewe leo unakuja unamlipisha kodi.

“Hutakiwi kuwa na akili ya darasa la tatu kujua kwamba huu msaada ni kwa walimu waliowafundisha wao na wanaofundisha watoto wao.

“Unatoza kodi inaenda kununua tena meza za walimu na vifaa vya kufundishia. Hayo ni mahesabu gani? Wakiendelea ntaenda kuwashitaki kwa Rais,” alisema Makonda.

Hata baada ya kauli hiyo ya Makonda iliyokuja siku chache baada ya kudai kuwa hatambui makontena hayo, TRA iliendelea na taratibu na Agosti 25 makontena hayo yalipigwa mnada na kukosa wateja.

Baada ya taarifa za makontena hayo aliyosema yana samani za shule za Dar es Salaam kukosa wateja kusambaa, Makonda alijitokeza kanisani akiwa Ngara mkoani Kagera na kusema mtu atakayeyanunua atalaaniwa na Mungu.

“Wananchi na vyombo vya habari wamejitolea na kuendelea kuhamasisha, huku walimu wakichanga kama sehemu ya kujikomboa, leo Mamlaka ya Mapato Tanzania wameamua kuuza samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe ili walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi.

“Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu, kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea kwa sababu Mungu ndiye aliyewawezesha watu wakakubali kujitolea.

“Nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwa kuwa vya madhabahuni havichezewi.

“Hivi ni vifaa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mungu hakunipa kwa ajili ya baa wala kumbi za starehe,” alisema Makonda.

 

  1. MPANGO ALIVYOJIBU MAPIGO

Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango, akiwa katika ziara bandarini, alimjibu huku akisema makontena hayo yatapigwa mnada hadi mteja atakapopatikana.

“Niliapa kutekeleza sheria za nchi na sheria za kodi. Katika usimamizi wa sheria hizi, kamishna zisimamie bila kuyumba. Piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadiri sheria inavyokuruhusu.

“Sheria inasema mzigo ulioagizwa kutoka nje hauna msamaha wa kodi. Hivyo, mchakato ulioanza kuutekeleza endeleeni nao,” alisema Dk, Mpango akimwelekeza Kamishna wa Forodha, Ben Usaji.

Dk. Mpango alisema; “Niwaombe viongozi wenzangu serikalini tuchuje maneno. Nawaomba Watanzania, anayetaka kuja kununua samani hizi asiogope, aje kununua.

“Haipendezi kusikia eti mtu atakayenunua samani hizi atapata laana, tena ya Mungu. Kwanini tunahusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii? Nawaomba Watanzania anayetaka kuja kununua samani hizi aje, hakuna cha laana wala nini.

“Kamishna piga mnada mara ya kwanza, ya pili, ya tatu kadiri sheria inavyokuruhusu. Hata mimi ningekuwa na hela ningekuja kununua tuone hiyo laana inatoka wapi.”

Kuhusu kauli ya Makonda kuwa samani hizo ni kwa ajili ya ofisi za walimu, Dk. Mpango alisema Serikali inathamini mchango wao na inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inaboresha mazingira yao ya kazi.

“Tuliapa kusimamia sheria. Sheria za kodi mimi ndiye mwenye dhamana, hivyo niulizeni niwajibu. Si sahihi hata kidogo kuingilia utaratibu ambao umebainishwa kisheria. Kamishna endelea kupiga mnada mpaka kieleweke,” alisema.

Waziri Mpango alisema sheria haitoi msamaha kwa samani kutoka nje na kila anayeziagiza anapaswa kufahamu hilo.

“Nimejizuia sana kujibizana kwenye mitandao, hii si hulka yangu, lakini haya ndiyo maelekezo ya Serikali,” alisema Dk. Mpango.

 

HISTORIA YA MAKONTENA

Sakata la makontena hayo lilianza baada ya tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, mwaka huu, likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia kodi.

Tangazo hilo lilionyesha TRA inakusudia kufanya mnada wa wazi Juni kwa mizigo iliyokaa bandarini kwa muda mrefu bila kukombolewa, ikiwamo ya Makonda.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye, wamiliki walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.

Tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD) yakiwa na samani.

Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa Makonda ndiye mwenye makontena hayo wakati huo, Februari 16 mkuu huyo wa mkoa alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la HabariLeo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa. Mzigo huo ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36.

Samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni 2, zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles