29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amchoka Sefue ndani ya siku 60

4(16)*Amng’oa ikulu, mikoba yachukuliwa na Balozi kijazi

*Atakumbukwa kwa kubeba mafaili utumbuaji majipu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amemng’oa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuhudumu katika wadhifa huo, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi Sefue amehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 65 tangu alipoteuliwa na Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana.

Hatua hiyo ya kuondolewa katika nafasi hiyo ya kiranja wa makatibu wakuu wa wizara, imekuja siku chache baada ya gazeti moja la wiki kuripoti juu ya kashfa na kumuhusisha Balozi Sefue na ufisadi katika miradi kadhaa ya maendeleo.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Rais Magufuli, amemteua Balozi Mhandisi John Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Kabla ya uteuzi huo, Kijazi alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India ambapo miaka ya nyuma wakati Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi, Balozi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

“Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue atapangiwa kazi nyingine,” ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Siku 65 Ikulu

Desemba 30, mwaka jana Rais Dk. Magufuli, alifanya uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wa wizara mbalimbali.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli, alimtangaza Balozi Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ambapo wadhifa huo amehudumu nao kwa siku 65 hadi kufikia jana kabla ya kutenguliwa.

Miaka minne ya utendaji wake

Balozi Sefue, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Desemba 30, mwaka 2011 akichukua nafasi ya Phillemon Luhanjo, ambaye alihitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma.

Kabla ya uteuzi wake Balozi sefue, alikuwa Balozi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa New York, Marekani.

Mbali na nafasi hiyo pia alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na pia alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada tangu Oktoba 2005 na aliapishwa Desemba 31, mwaka 2011.

Tangu wakati huo hadi kufikia jana Balozi Sefue, alihudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne na siku 65.

Wasifu wa Balozi Kijazi

Alipata shahada ya kwanza ya heshima ya Uhandisi Ujenzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhandisi Barabara kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham,  Uingereza.

Mwaka 1982 hadi 1986 alifanya kazi kama Mhandisi Mtendaji Msaidizi katika Wizara ya Ujenzi na mwaka 1986 hadi 1996 kama Mhandisi wa Mkoa, katika Wizara ya Ujenzi.

Aidha mwaka 1996 hadi 1999 alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Matengenezo ya Barabara, Wizara ya Ujenzi kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa kuanzia mwaka 1999 hadi 2002 katika wizara hiyo. Akateuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, mwaka 2002 hadi 2005, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Miundo Mbinu Januari hadi Novemba 2006.

Desemba 2006 hadi Juni 2007 aliteuliwa kufanya Shughuli maalumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa JGTS, Tanzania.

Juni 2007 akateuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini India na Mei 27, 2013 akawa balozi nchini Singapore.

Sefue na majalada ya majipu

Kila wakati yalipokuwa yakitangazwa kutumbuliwa majipu, aliyekuwa akijitokeza kutangaza uamuzi wa Rais Magufuli ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Kutokana na kasi hiyo ambayo imewakumba vigogo kadhaa wakiwemo wale wa Mamlaka  ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Uamuzi huyo ambao ulitangazwa na Balozi Sefue ni wa kutengua uteuzi na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo,  Dickson  Maimu na wenzake wanne.

Katika mkutano wake na wanahabari Balozi Sefue, alisema Rais amechukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya matumizi ya Sh bilioni 179.6 kiasi ambacho alisema ni kikubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanywa na NIDA.

Mbali na Maimu,   waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande,  Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli ilitekelezwa siku chache baada ya kufuta uteuzi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk. Feisail Issa, ambaye ilidaiwa alitaka kupigana na Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo.

KIPANDE ‘OUT’

Rais Dk. Magufuli pia  alitengua uteuzi wa  Madeni Kipande kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.

Balozi Sefue alisema uteuzi wa Kipande umetenguliwa kabla muda wake wa majaribio haujaisha wa miezi sita  kwa vile amebainika kuwa na utendaji mbovu.

MABALOZI WARUDISHWA

Katibu Mkuu Kiongozi pia alisema Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa, kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha.

“Leo hii (jana) mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa mafisa wakuu au waandamizi ambao wako chini yao,” alisema Balozi Sefue.

Mabalozi hao kuwa ni Dk. Batilda   Buriani, aliyeko Tokyo    Japan na Dk. James Msekela, aliyeko Rome, Italia.

Alisema pia Rais Magufuli   amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe. Amerejeshwa  Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ambako atapangiwa kazi nyingine.

MAELEKEZO KWA WATUMISHI

Kila wakati Balozi Sefue, akiwa anahudumu katika nafasi hiyo aliwataka viongozi na watumishi wa umma kubadilika kwa dhati katika  utendaji wao na kuwa waadilifu huku akiagiza watumishi wote  kuvaa majina yao wanapokuwa kazini.

“Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao   iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya ovyo,” alisema.

VIGOGO 100 WANG’OLEWA

Tangu Rais Magufuli alipoapishwa Novemba 5,  mwaka jana Serikali yake imewaondoa kazini takribani vigogo 100 wa Serikali ya awamu ya nne.

Hatua hiyo inaelezwa ni miongoni mwa  mkakati wa kuzika mfumo wa Serikali ya awamu ya nne ambao baadhi ya vigogo walikuwa wakifanya mambo holela na kusahau wajibu wao kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hatua hizo za kinidhamu kwa idadi kubwa ya watumishi wa Serikali,  inaonyesha kuwa kila siku kuna wastani wa vigogo wawili    watendaji wa juu ambao wamejikuta wakifutwa kazi  kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutumia madaraka vibaya na hata kuisababishia hasara Serikali.

Fagio hilo   linajumuisha watumishi wa Serikali waliosimamishwa kazi kutoka kwenye taasisi mbalimbali pamoja na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa.

Asilimia kubwa ya vigogo waliosimamishwa kazi walichukuliwa hatua na Rais mwenyewe na wengine Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku wawili kati yao wakiwajibishwa na mawaziri husika katika wizara wanazoongoza.

RELI

Mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli  alitangaza kufuta uteuzi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO),  Benhadard Tito na kuvunja bodi yake ya wajumbe wanane  na ile ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) yenye wajumbe wanane pia.

Ilidaiwa kuwa TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 mabovu huku yakiligharimu taifa Sh bilioni 220.

TAKUKURU

Desemba 16,  Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(Takukuru), Dk. Edward Hosea, baada ya kujiridhisha kuwa alishindwa kushughulia matatizo ya rushwa na pia ameshindwa kuendana na kasi ya Dk. Magufuli.

Mbali na Dk. Hosea, watumishi wengine wanne wa Takukuru walisimamishwa kazi kwa kukiuka agizo la Rais, kwa kusafiri kwenda nje ya nchi bila kibali maalumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles