26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aahidi mambo saba Kigoma

 NORA DAMIAN-KIGOMA

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameahidi kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati inayojumuisha viwanja vya ndege, bandari na kuboresha huduma za usafiri wa anga na kwenye maziwa akiwataka wakazi wa Kigoma wakae mkao wa kutengeneza biashara.

Akizungumza jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Lake Tanganyika alisema ana mipango mikubwa kwa ajili ya mkoa wa Kigoma na kuwaomba Watanzania wamchague aubadilishe.

Alisema mji wa Kigoma ni miongoni mwa miji minane iliyo kwenye mradi wa uboreshaji miji ya kimkakati unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Sh bilioni 799.52 lakini akashangaa pamoja na juhudi hizo watu wengine wanajitokeza na kubeza kuwa Serikali haijafanya kitu.

Miji mingine ni Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Tanga, Mikindani – Mtwara na Ilemela – Mwanza.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli kupitia mradi huo wamejenga kilomita 15.13, limejengwa dampo la kisasa katika eneo la Msimba, mifereji na uwekaji wa taa za barabarani kwa gharama ya Sh bilioni 31.19.

“Mradi huu ulikuwa kwenye ilani ya miaka mitano iliyopita na wala sikununa kwamba kwa sababu Kigoma hamkuchagua CCM…nilisema ni lazima tuufanyie kazi sisi hatuna ubaguzi tunawapenda Watanzania wote.

“Mtu anakwambia nimeuleta mradi huu maana yake aliupeleka yeye Dodoma, tujiepushe na matapeli wa siasa, kwenye siasa matapeli wapo. Kwahiyo ukiona taa hapa barabarani mtu asije akasimama akatafuta umaarufu kwa sababu tunaweka na maeneo mengine.

“Arusha mbunge alikuwa wa Chadema lakini tulipeleka mradi huu tumetumia karibu Sh bilioni 600, Mikindani (Mtwara) mbunge alikuwa wa CUF nako pia tumepeleka…hii ndiyo dhana halisi kwamba maendeleo hayana chama, niliamua nilaumiwe ili nitoe upendeleo wa dhati kwa wananchi wa Kigoma,”alisema Dk. Magufuli.

AHADI MPYA

Dk. Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wamepanga kuendelea kuboresha usafiri katika Ziwa Tanganyika ambapo wametenga Sh bilioni 10 kukarabati meli ya MV Liemba, MT Sangara (Sh bilioni sita), kununua meli mbili kubwa ambapo moja itakuwa ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 400 na nyingine itakayobeba abiria 600 na tani 400.

“Mimi sitoi ahadi hewa, nataka watu wafanye biashara, nataka Kigoma niifungue nimechoka kusikia ajali kwenye Ziwa Tanganyika lazima hili likome, tunataka tuwe na mwelekeo wa kutengeneza Kigoma mpya,” alisema.

Aidha aliahidi kuwa Bandari ya Kigoma itaboreshwa na kuwa ofisi kuu ya kuhudumia bandari zote za Ziwa Tanganyika pamoja na kujenga ghala la kuhifadhia mizigo.

Katika sekta ya anga Dk. Magufuli alisema kutafanyika upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege Kigoma ili kuimarisha usafiri huo na kukuza sekta nyingine ikiwemo ya utalii.

“Tunaambiwa tukinunua ndege ni rakshari yale ni mawazo yaliyopotoka, tunataka watalii wanaokwenda Arusha na Kilimanjaro idadi ile ile waje Kigoma na kuongeza fursa za ajira, miaka mitano iliyopita sekta hii imeajiri watu milioni nne,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema pia upanuzi wa uwanja huo utahusisha ujenzi wa jengo la ghorofa la abiria pamoja na uwekaji taa.

Kwa upande wa maji alisema mahitaji ya maji katika mkoa huo ni lita za ujazo milioni 23 na kwamba mradi unaoendelea sasa utazalisha lita milioni 40 hivyo kumaliza changamoto ya ukosefu wa maji katika maeneo mengi ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli pia kuna mradi unaotekelezwa vijijini unaogharimu Sh bilioni 13 na kwamba katika bajeti ya 2020/21 wametenga Sh bilioni 24.12 kushughulikia kero ya maji katika wilaya mbalimbali za Kigoma.

“Umeme vimebaki vijiji 113 lakini tuna mipango ya kumalizia vijiji vilivyobaki kwa kuunganisha mkoa wa Kigoma kwenye gridi ya taifa,” alisema.

Akizungumzia zao la mchikichi alisema miaka ya nyuma lilionekana limesahaulika na kwamba ataendelea kulifufua sambamba na kutafuta masoko wananchi wa Kigoma waweze kufaidika.

“Nilimtuma waziri mkuu hapa nilimpa kazi hiyo ya kufufua kwa sababu nataka Kigoma ipande juu, nikaanza kufufua mashamba ya JKT…kwahiyo nikituma mtu akishafanya vizuri mwingine anajitokeza pale,” alisema.

Dk. Magufuli pia alisema wanaendelea na ujenzi wa hospitali katika wilaya za Kigoma na Kakonko, kukarabati vituo 11 na zahanati 41.

Alisema pia wametenga Sh bilioni 567 katika miradi ya barabara ikiwemo ya Nyakanazi – Kibondo (kilomita 50) ili katika kipindi kifupi kijacho kusiwe na shida ya barabara.

“Tuna mipango mikubwa kwa ajili ya Kigoma tunaomba mtupe kura za kutosha, tunataka Kigoma tuibadilishe…tufanye mabadiliko mwaka huu, mnifurahishe kwelikweli mnichagulie wabunge, madiwani wa CCM na mimi mwenyewe mnipe kura za kutosha,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles