Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Rais John Magufuli ameagiza Kikotoo kilichokuwa kinatumika kwa kila mfuko kabla ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuunganishawa kindelee kwa kipindi cha mpito cha miaka mitano hadi 2023.
Kumekuwepo na mjadala kuhusu mafao baada ya kanuni za Usimamizi wa Mifuko ya Jamii kuondoa mfumo wa zamani wa kulipa asilimia 50 ya mafao kwa mkupuo na asilimia 75 itolewe kama pensheni kwa kila mwezi kwa kipindi chote cha maisha ya mstaafu.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Ijumaa Desemba 28, Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA),Watendaji wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya (PSPF na NSSF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA)walipokutana kujadili masuala yahusuyo mafao ya wafanyakazi hususani Kikotoo.
“Kustaafu sio dhambi, kustaafu ni heshima na mstaafu anatakiwa aheshimiwe, mtu anastaafu akiwa amefanya kazi muda mrefu halafu umwambie achukue fedha zake kidogokidogo kwa kigezo eti itamsaidia anavyoendelea kuishi, we nani kakuambia ataishi miaka mingapi.
“Nimeamua kuwe na kipindi cha mpito na kile kikotoo kilichokuwa kinatumika kwa kila mfuko kabla ya mfuko kuunganishwa, kiendelee kutumika hadi 2023, “ amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ametoa wito kwa Watendaji na wenyeviti wa mifuko hiyo kujitafakari na kuacha kuwekeza katika miradi isiyozalisha na kutumia fedha za wanachama bila ridhaa yao.