26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Joto la uchaguzi lapanda CCM

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

WAKATI mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba ukitarajiwa kuanza kesho, joto linaonekana kuanza kupanda.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, mchuano mkali unatarajiwa kuwa ndani ya chama haswa kwenye nafasi ya Urais wa Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Ratiba iliyotangazwa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, imegeuzwa kuwa ajenda katika mitandao ya kijamii huku wengi wakihoji iwapo wataibuka wanachama watakaotaka kupambana na Rais Dk. John Magufuli ambaye anatarajiwa kuomba tena ridhaa ya chama chake kuwania ngwe ya pili.

Hata hivyo hali hiyo haitarajiwi sana kwasababu CCM ina utaratibu wa kumpitisha rais anayemaliza muhula wake wa kwanza kugombea tena miaka mitano bila kupingwa.

Kwa upande wa Zanzibar kumekuwa na mjadala nani atapewa kijiti cha kumrithi Rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein, anayemaliza kipindi chake cha pili hasa baada ya kuwapo wanasiasa mbalimbali wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo.

Katika dakika za lala salama wanaotajwa kugombea wamekuwa wakipigana vikumbo huku baadhi yao wakitumia upepo wa shughuli mbalimbali kujinadi kiaina na wengine wakionekana kufanya harakati za kimya kimya ili kujitengenezea mtaji wa kura katika vikao vya ndani ya chama.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa, “huku Bara hakuna shida kazi imeshaisha, gumzo liko Zanzibar subirini.”

Rekodi zinaonyesha mbali ya Dk. Shein marais wengine waliowahi kuiongoza Zanzibar ni Sheikh Abeid Amani Karume (1964-1972),  Sheikh Mwinyi Aboud Jumbe (1972-1984), Ali Hassani Mwinyi (1984-1985), Idris Abdul Wakili (1985-1990), Salmin Amour (1990-2000) na Amani Abeid Karume (2000-2010).

Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume,  alipata wadhifa huo baada ya kutokea mapinduzi yaliyosababisha kupinduliwa kwa Sultani wa mwisho wa Sultan Jamshid bin Abdullah Januari 1964.

Miezi mitatu baadaye, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzishwa na Karume akawa makamu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais.

Jina la Karume lilirejea tena baada ya Amani Abeid (mtoto wa Karume) kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na kuingia madarakani Novemba 2000 hadi Novemba 2010.

WANAOTAJWA ZANZIBAR

Miongoni mwa wanaotajwa kuwania urais Zanzibar ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi Ali Karume, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na Waziri wa Viwanda upande wa Zanzibar, Balozi Amina Ali ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alijitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais wa Jumuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika orodha hiyo yumo pia aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo Machi 3 mwaka huu baada ya kile kilichoelezwa kukaidi agizo la chama chake la kutoanza kampeni kabla ya wakati.

Mbali na hao, pia wanatajwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo Agosti 26, mwaka huu, Samia alisema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

urais Zanzibar.

UBUNGE, UDIWANI UWAKILISHI

Kulingana na ratiba iliyotolewa juzi wanaotaka kugombea ubunge, uwakilishi, udiwani na viti maalumu watachukua na kurejesha fomu Julai 14 hadi 17 mwaka huu.

Wanachofanya makada wengi hivi sasa hasa wale wanaotajwa kutaka kugombea nafasi hizo ni kutafuta ushawishi au ‘kiki’ ya kuwafanya waonekane ili kujitengenezea mtaji wakati wa vikao vya ndani na nje ya CCM. 

Wengine wamekuwa wakiitumia kwa kasi mitandao ya kijamii kujipambanua kwa kueleza yale waliyotekeleza wakati wakiomba kura mwaka 2015.

Wamo pia baadhi ya wabunge wa kuteuliwa na wale wa Viti Maalumu ambao pia ni mawaziri wameonyesha dalili ya kutaka kugombea majimbo mbalimbali.

Mapema wiki hii wakati akihitimisha hotuba ya Makadirio ya Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa alisema; “Watanzania msisahau kumpatia rais wetu wabunge na madiwani wanaomudu maadili na mwendo wa Hapa Kazi Tu…na kama itawapendeza wananchi wenzangu wa Buhingwe na chama chetu (CCM) basi iwe pamoja na mimi mtumishi wenu.

Jimbo la Buhingwe kwa sasa linaongozwa na Albert Obama.

Katika kile kinachoonekana ni kumjibu Dk Mpango,  Obama, wakati akichangia bajeti hiyo alisema wananchi wa Buhingwe wanajua alipowatoa na atakapowapeleka na ana imani atapitishwa tena na CCM kugombea jimbo hilo.

“Ukija kwenye orodha ya majina yangu bungeni utaambiwa Obama anaitwa nani, utaambiwa ni mashine ya jimbo, mashine ya kusaga na kukoboa, jina la nne utakaloambiwa kwangu ni simba wa yuda la mwisho ni katapila.

“Naomba hayo majina yawe katika ‘hansard’ ya Bunge, Buhingwe wanajua tulikotoka, tuliko na tunakoelekea. Niseme 2020 Magufuli hapa, Obama hapa,” alisema Obama.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema uamuzi wa baadhi ya wabunge wa kuteuliwa na wale wa viti maalumu kuamua kuingia ‘mzima mzima’ katika kinyang’anyiro hicho unachochewa pia na rekodi zao za kiutendaji.

RATIBA ILIVYO

Kwa mujibu wa Polepole, kwa upande wa Tanzania Bara tukio la kwanza litakuwa ni uchukuaji fomu kwa nafasi ya kiti cha urais, litakaloanza Juni 15 hadi 30 mwaka huu.

Alisema tukio la pili ambalo litakwenda sambamba na muda huo wa siku 15 ni utafutaji wa wadhamini mikoani.

Alisema tukio la tatu litakuwa ni vikao vya uchujaji, ambapo Julai 6 hadi 7 mwaka huu, kitaketi kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kitakachoanzisha mchakato wa uchujaji, kisha Julai 8 mwaka huu kitaketi kikao cha Kamati ya Usalama na Madili ya Taifa chama hicho.

“Julai 9 mwaka huu, kitaketi Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ambacho kitatoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano, wanaoomba kugombea nafasi hiyo ya urais,”alisema Polepole.

Vilevile Polepole alisema Julai 10 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kitapendekeza kwa Mkutano Mkuu wa CCM, majina yasiyozidi matatu ya wanachama wa chama hicho, wanaoomba kugombea urais.

Katibu huyo wa itikadi na uenezi wa CCM, alisema Julai 11 hadi 12 mwaka huu, Mkutano Mkuu wa CCM Taifa utachagua jina moja la mgombea wa urais wa Tanzania.

ZANZIBAR

Kwa upande wa Zanzibar, Polepole alisema Juni 15 hadi 30 mwaka huu itakuwa ni tukio la uchukuaji fomu na kurejesha.

“Juni 15 hadi 30 mwaka huu, kutafuta wadhamini mikoani, baada ya hapo vitafuata vikao vya uchujaji, Julai 1 hadi 2 mwaka huu, itaketi Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, Julai 3 kitaketi kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar,”alisema Polepole.

Polepole alisema Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM kitakuwa Julai 4 mwaka huu kwa ajili ya kutoa mapendekezo juu ya wanachama waliojitokeza kuomba kugombea urais wa Zanzibar.

“Kikao hicho kitafuatiwa na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa kitakachoketi Julai 9 kwa ajili ya kupendekeza majina matatu ya wanachama wanaoomba kugombea kiti hicho. Kisha, Julai 10 mwaka huu, Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM kitachagua jina moja la mgombea.

Aidha alisema Julai 11 hadi 12, Mkutano Mkuu wa CCM taifa utaketi kwa ajili ya kuthibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles