JPM ateta na Rais Mteule Burundi, ampongeza Mahakama kuagiza aapishwe

0
836

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya vyombo vya habari vya kimataifa kuripoti tetesi kwamba Rais Mteule Burundi, Evariste Ndayishimiye mgonjwa, Rais Dk. John Magufuli amezungumza naye kwa njia ya simu.

Zaidi Rais Magufuli amempongeza kwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba nchini Burundi iliyoagiza Rais huyo mteule aapishwe haraka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson  Msigwa, katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemtakia heri Ndayishimiye kuelekea kuapishwa kwake  hivi karibuni kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi

Rais Magufuli amemhakikishia Ndayishimiye kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na Burundi kwa kuwa nchi hizo ni majirani, marafiki na ndugu wa kihistoria.

Rais Magufuli amerudia kumpa pole kwa msiba wa kuondokewa na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia Juni 09, 2020.

Amemueleza kuwa yeye na Watanzania wote wanaungana na Warundi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Amemuomba kufikisha salamu zake za rambirambi kwa Warundi wote na kuwasihi waendelee kuwa watulivu na wastahimilivu.

Kabla ya uamuzi huo wa Mahakama ya Burundi kuagiza Rais huyo mteule aapishwe haraka juzi  Baraza la Mawaziri nchini humo lilisema litaongoza nchi hiyo hadi rais mpya atakapoapishwa.

Uamuzi huo ulifikiwa kufuatia mkutano uliyofanywa siku ya Alhamisi chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa kwanza Gaston Sindimwo.

Wakati Baraza hilo la Mawaziri likifikia uamuzi huo kabla ya ule wa mahakama, Katiba ya nchini Burundi inaonyesha wazi kuwa Spika wa Bunge la kitaifa, Pascal Nyabenda alitakiwa kuapishwa kushikilia wadhifa wa Rais kwa kipindi cha mpito hadi Rais Mteule atakapoapishwa rasmi kuchukua hatamu ya uongozi.

Awali kabla ya kifo cha Rais Nkurunziza, rais huyo mteule ilikuwa aapishwe mwezi Agosti baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwezi Mei.

Juzi pia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC liliripoti taarifa ambazo ilisema hazijathitibitishwa zilizoeleza kuwa Rais huyo Mteule, Jenerali Évariste Ndayishimiye, pia ni mgonjwa.

Taarifa hizo zilieleza kuwa mke tu ndiye aliyeonekana na  alipigwa picha akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Rais

Ndayishimiye lakini rais huyo mteule hajaonekana hadharani

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here