26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jonesia kuchezesha Afcon ya wanawake Ghana

na mwandishi wetu-dar es salaam

MWAMUZI wa Tanzania, Jonesia Rukyaa, amechaguliwa kuchezesha Fainali za Afrika za Wanawake zitakazofanyika nchini Ghana mwaka huu.

Jonesia amechaguliwa katika orodha ya waamuzi wa katikati akiwa ni Mtanzania pekee katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Novemba 17 hadi Desemba 1, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema Rukyaa amechaguliwa katika orodha ya waamuzi 13 wa katikati na wasaidizi 12.

“Fainali hizo zitatumika kupata timu tatu zitakazowakilisha Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia kwa wanawake itakayofanyika  mwakani Ufaransa,” alisema.

Jonesia amekuwa  akipata nafasi katika michuano mbalimbali ya kimataifa, Februari mwaka huu, alichezesha mashindano ya wanawake Ureno yaliyojulikana kwa jina la Algarve.

Mwaka 2016 alikuwa mwamuzi wa akiba kwenye mashindano kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake wenye umri chini ya miaka 17, Sierra Leone.

Michuano hiyo inashirikisha nchi nane zilizopangwa katika  makundi mawili,  A likiwa na mwenyeji Ghana, Algeria, Mali na Cameroon, kundi B ni Nigeria, Afrika Kusini, Zambia na Kenya.

Katika hatua nyingine Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi ilikutana juzi na kupitia matukio mbalimbali yaliyojitokeza ikiwa pamoja na malalamiko yaliyopelekwa.

Alisema katika mechi ya Azam dhidi ya African Lyon, mwamuzi Fikirini Yussuph, amepewa onyo baada ya kuonekana umakini wake kuwa mdogo.

Mechi kati ya Mwadui FC na  Ruvu Shooting, kocha wa Ruvu Shooting alitolewa katika benchi na mwamuzi kwa kosa la kupinga maamuzi ya mwamuzi, hivyo kamati iliamua kumfungia mechi mbili na faini ya Sh laki tano.

Wambura alisema mechi kati Yanga na  Alliance, wageni ambao ni Alliance walipita katika njia ambazo si sahihi  hivyo wamepigwa faini ya Sh laki 5.

“Mechi nyingine kati ya Azam FC dhidi ya JKT Tanzania, mchezaji wa Azam FC, Ennock Atta, alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga teke kwa makusudi mchezaji wa JKT Tanzania,  kwa mujibu wa kanuni ya 38 (9) inayohusiana na udhibiti wa wachezaji amefungiwa mechi tatu na faini ya shilingi laki tano,” alisema.

Alisema mchezo mwingine  kati ya Coastal Union na  Kagera Sugar, wenyeji Coastal wamepewa onyo kwa kuchelewa kufika kwa zaidi ya robo saa hivyo wamepewa onyo, mchezo  kati ya Ndanda FC dhidi ya Biashara United, mchezaji wa Ndanda FC, Masoud Abdallah, alipewa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga mpinzani hivyo amefungiwa mechi tatu na faini ya Sh laki tano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles