26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

JK:Ole wao wagombea CCM

Pg 1SHABANI MATUTU, SONGEA na Oliver Oswald (Dar)
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewaonya watu wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho.
Amesema endapo watavunja sheria na kanuni wasikilaumu chama hicho bali wajilaumu wenyewe.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Songea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 38 ya CCM yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Alisema anaamini CCM ni chama kinachofuata taratibu za kuwapata viongozi wake bora kwa kutumia vikao vyake rasmi vinavyowateua ambavyo hukaa Dodoma.
Alisema taratibu na kanuni za chama hicho kumpata mgombea zipo wazi na kuwa atakayechaguliwa, kila mtu atakayemsikia atasema “naam huyu ndiye’ na siyo yule ambaye akitangazwa watu wataanza kuguna.
“Oktoba mwaka huu utafanyika Uchaguzi Mkuu na kuchagua rais wa awamu wa tano, bila shaka atakuwa ni Rais anayetoka CCM. Tunataka tukimtangaza mgombea wetu katika ukumbi mpya pale Dodoma, maana wakati wangu ule ilikuwa Chimwaga.
“Baada ya kumtangaza tu, Watanzania wataseme hapo barabara. Kama hawapo wanaosikika sasa nendeni na mshawishi watu wazuri maana CCM ina ‘material’ ya watu wazuri.
“Maana nami leo sasa natoa siri, siku moja alikuja Kinana akanimbia amekuja muasisi mmoja, je umemuona? Nikamjibu sijamuona.
“… basi akanimbia sawa kama umemuona au hukumuona sawa lakini we zingatia ujumbe wake. Nami ninachotaka kusema CCM tuna utaratibu tumeweka wa kuteua wagombea kwa kuzingatia kanuni na taratibu na maadili ya chama chetu,” alisema.
Rais Kikwete, kila mara alikuwa akinukuu kauli mbalimbali za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, ikiwamo aliyosema kuwa rais anaweza kutoka chama chochote lakini rais bora atatoka CCM.
“Hivyo kama hatutomchagua anayefaa tutakuwa tumemuangusha muasisi wetu na chama. Mwalimu alitueleza kwamba bila CCM imara tutayumba hivyo tusikubali kufanya vitendo kinyume na wosia huu ili nchi isiyumbe.
“Ngoja niwape siri lakini si zote… Siku moja mzee mmoja tulikutana aliniambia maneno fulani nikamkatalia na baadaye nikakutana na Kinana akaniuliza kama nimemuona mzee huyo nikamwambia sikumuona akaniambia nitafakari maneno yake.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema si dhambi kwa mtu kujitokeza na kutaka urais lakini ni vema maadili ya chama yafuatwe kwa wagombea kuliko kwenda kinyume na miiko na maadili ya chama.
“Si dhambi kwa mtu kujitokeza na kuutaka urais bali tunataka maadili yafuatwe, hivyo wagombea mnatakiwa kufuata maadili ya chama na asiyefuata asije kutulaumu.
“Na katika hili hakutaharibika jambo, tutateua wagombea ambao Watanzania hawatakuwa na kigugumizi. Kwa hali hiyo wagombea ni lazima wazingatie masharti ya chama, asiyezingatia hayo asiilaumu CCM, ajilaumu mwenyewe.
Awafunda viongozi
Rais Kikwete amekitabiria CCM kufanya vizuri huku akitoa angalizo kwa chama hicho kutobweteka kwa sababu anaamini kitakumbana na changamoto kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema katika uchaguzi huo CCM kitashinda kama kilivyafanya katika uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 .
“Naamini mwaka huu wapinzani hawana chao hivyo tutashinda kwa roho baridi, ila wana-CCM wanatakiwa kutobweteka na maneno yangu… kwani uchaguzi huu unaweza kuwa na changamoto kubwa kutoka kwa wapinzani wetu wa Ukawa,” alisema.
Rais Kikwete alieleza mbinu za kukabiliana na changamoto za Ukawa kuwa ni kuhakikisha wana CCM wanakuwa na umoja wa dhati wa kukipigania chama katika uchaguzi wa udiwani, ubunge na urais wa Muungano pamoja na wa Zanzibar.
Mbinu nyingine alisema ni viongozi kutimiza ahadi walizotoa wakati wa uchaguzi na baada ya kushinda uchaguzi huo kwa sababu suala la kutotimiza ahadi linaweza kupunguza ushindi wa chama hicho.

“Mwaka huu hakuna kulala hivyo tunatakiwa kukutana mara kwa mara na kuhakikisha tunaweza kushawishi makundi mbalimbali kuingia chamani wakiwamo vijana, akina mama na wazee,” alisema.
Alisema iwapo yatakuwapo maandalizi mazuri yatasaidia kukirahisishia kupata ushindi usiokuwa na jasho.
Alitoa wito kwa wilaya na mikoa ambazo hazijatimiza agizo la chama la kuanzisha mifuko ya uchaguzi zifanye hivyo akitoa tahadhari ya kutochukua fedha za moto.
Kikwete aliwataka viongozi wa chama hicho kuiga mfano wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kwa kufanya mikutano mingi ya kukipigania chama.
“Chama chetu kama vingine hatuna budi kufanya mikutano ya kuwashawishi wanachama kujiunga nacho ikiwamo kujitokeza katika upigaji wa kura ambako kwa sasa mnatakiwa kujiandikisha kwa ajili ya kupata kadi mpya ambazo zitawasaidia kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu na Katiba Inayopendekezwa,” alisema Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kutekeleza hatua ya uandikishaji kwa utaratibu wa BVR katikati ya Februari mwaka huu.

…Katiba Inayopendekezwa itapita
Rais Kikwete alisema anaamini Katiba Inayopendekezwa itapita Aprili 30 hata kama Ukawa wanapambana kupiga kampeni ya kuihujumu kupigiwa kura ya Hapana.
Alisema suala la muhimu kwa sasa ni kuhakikisha Katiba hiyo Inayopendekezwa inatangazwa katika magazeti na vipeperushi ikiwamo kwa CCM kutoa elimu chanya tofauti na Ukawa aliosema wanatoa elimu hasi ili ikataliwe.
“Katika historia ya Tanzania hatujawahi kuwa na Katiba nzuri inayojali masilahi ya makundi mbalimbali wakiwamo vijana, walemavu, wanawake, wazee, watoto ikiwamo na kushughulikia kero za Muungano,” alisema.
Alisema pamoja na Ukawa kutangaza kususia mchakato huo taratibu nyingine zitaendelea kama zilivyopangwa ikiwamo kuhahakikisha Watanzania wanakuwa na Katiba bora.
Akinukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Rais Kikwete alisema ‘Usisonge ugali kabla maji hayajachemka’ huku akiweka wazi kuwa suala la kuwa na Serikali tatu bado halijafika kama wanavyotaka baadhi ya watu.
“Njia sahihi ya kuonyesha hili ni kushiriki kura ya maoni… mkisusia sisi tutashinda,” alisema.
Rais Kikwete alisema ana imani kwamba kura ya Ndiyo itashinda kwa kishindo wakati wa upigaji wa kura Aprili 30, mwaka huu .
“Kwa sasa maji ya Serikali tatu bado hayajachemka kwa hiyo sioni sababu ya wapinzani kuanza kushawishi wananchi kuikataa Katiba Inayopendekezwa wakati mchakato wa kupiga kura ya maoni upo njiani unakuja.
“Mimi nawaachia wananchi ndiyo watathibitisha kwa kupiga kura ya ndiyo kwani mahitaji yote muhimu yamo ndani ya Katiba Inayopendekezwa, kwa hiyo hao wanaosusa waache wasuse ila nyie jitokezeni kupiga kura ya maoni,”alisema Kikwete.
Lowassa ang’ara
Eakati huohuo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliteka nyoyo za wakazi wa mji wa Songea baada ya kuingia katika Uwanja wa Majimaji na kushangiliwa kwa nguvu na umati mkubwa wa makada wa CCM.
Tukio la kushangiliwa kwa Lowassa katika sherehe hizo lilianzia katika uwanja wa ndege wa mjini Songea wakati alipowasili.
Kushangiliwa kwa Lowassa kulikuwa tofauti na viongozi wengine wa chama hicho waliotangulia kwa vile yeye alishangiliwa kwa muda mrefu huku muda wote yeye akiwa anawapungua mikono wananchi kushoto na kulia mwa uwanja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles