Tunu Nassoro-Dar es Salaam
RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete, amesema cheo alichokuwanacho Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Usalama wa Taifa, marehemu Apson Mwang’onda, hakikumpa jeuri na kiburi.
Akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kuuaga mwili wa Mwang’onda iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam, Kikwete alisema mzee Apson alikuwa ni mkweli mwenye nidhamu na weledi wa hali ya juu.
Alisema Mwang’onda aliipenda kazi yake na kuifanya kwa ujasiri na moyo na kwa bidii zote.
“Alitimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kushari mambo kadhaa ya namna bora ya kuendesha nchi na hivyo kuwa kiungo muhimu katika uongozi,” alisema Kikwete.
Alisema alikuwa akiikosoa Serikali katika mambo mbayo imeteleza kwa kueleza kwa uwazi kilichokosewa.
“Alikuwa akinikosoa kila tulipokosea na kuniambia kuwa Serikali yako imefanya makosa haya, wala hakuwa na uoga,” alisema Kikwete.
Aliongeza alipoingia madarakani, Mwang’onda alimwambia yeye na wenzake watakuwa wakimshauri katika kutekeleza majukumu yake hivyo awe tayari kupokea ushauri hata kama utakuwa mbaya najiandae kuupokea.
“Nashukuru aliniandaa kisaikolojia kwani hata aliponiletea taarifa mbaya niliisoma na bahati nzuri alikuwa muungwana na ikiwa kubwa sana tulikaa wote na kujadiliana,” alisema Kikwete.
Alisema alimwomba amvumilie wakati wa kutekeleza majukumu yake ya kila siku katika idara hiyo.
Kikwete alisema hata Mwang’onda alipotaka kustaafu, alimwomba kumwongeza muda ili aweze kuendelea kufanya naye kazi.
“Alikubali na nilipotaka kumwongeza tena, alikataa na kusema anahitaji kustaafu na kuwaachia wengine. Alisema mwisho wake walio nyuma yake ambao wangeshika nafasi yake watastaafu yeye akiwa madarakani na hivyo kulazimika tuchukue wadogo zaidi wasio na uzoefu wa kuongoza,” alisema Kikwete.
Alisema marekemu ameacha alama katika taifa hasa mipango yake ya kuboresha na kuiendeleza idara ya usalama nchini.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na usalama mstaafu (CDF), George Waitara, alisema Mwang’onda alikuwa na ushirikiano mkubwa katika utendaji kazi wake.
Alisema walitengeneza ushirikiano wa watu watatu ambao walikuwa ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Katika ushirikiano wetu hatukuwa wanafiki wala wajeuri, tulifanya kazi kwa pamoja na hata tulipokutana tulijadili kuhusu amani ya nchi,” alisema Waitara.
Alisema Mwang’onda alikuwa ni msema ukweli hakusita kukosoa pale alipoona mambo hayaendi sawa.
“Hata alipostaafu alikuwa akiona jambo halijakaa vizuri aliniita na kunieleza huku akitoa ushauri katika masuala muhimu,” alisema Waitara.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Omary Mahita alisema walifanya kazi na Mwang’onga kwa zaidi ya miaka 23 ambapo miaka 10 wakiwa ni viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema walitekeleza mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama wakiwa na ushirikiano wa watu watatu, Waitara, mwang’onda na yeye.
“Mwang’onda alitekeleza majukumu yake kwa mawazo na vitendo hivyo kuturahisishia na sisi kazi zetu,” alisema Mahita.
Alisema alikuwa akitoa ushauri kwa viongozi wa nchi bila kuwa na woga na kutoa mwongozo na mawazo yake kiungwana.
“Binafsi nitamkumbuka kwa kuwa tulikuwa tukisaidiana katika mambo mbalimbali ya kijamii hasa pale nilipofiwa na baba yangu alinisaidia kusafirisha maiti kwenda Morogoro kwa maziko.
Katika msiba huo Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Abdurahman Kinana, alikuwa kivutio kwa wanahabari baada ya kutokuonekana kwa muda mrefu baada ya kutoa waraka uliokuwa ukiikosoa Serikali.
Waandishi wa habari walitaka kujua alikokuwa baada ya kutoa waraka huo huku wakimsonga ingawa hakuwa tayari kuzungumza.
Mwili wa Mwang’onda ulisafirishwa jana kwa ndege maalumu kuelekea Kijiji cha Old Vwawa ambako utafanyiwa maziko leo. Marehemu ameacha mjane na watoto watano.