Na Beatrice Kaiza, Mtanzania Digital
Vijana nchini wametakiwa kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere kwa kufanyakazi kwa bidii na kujifunza huku wakiendeleza ujamaa ambao aliusisitiza hasa katika kuinua kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Jumatano Juni 8, 2022 na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete wakati akifungua mdahalo katika Kongamano la 13 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).
Amesema miongoni mwa maono ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kuona Afrika inakua kimaendeleo na kumudu kujitegemea kiuchumi huku akiwataka vijana kutumia elimu yao kujikomboa kiuchumi.
Pia Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Prof.Rwekeza Mukandala amesema maarifa yanayotolewa katika Kigoda cha Mwalimu Nyerere yamedhamiria kuwajengea vijana kuwa na maisha ya kufanya kazi, kujituma na kujitolea.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema yale mawazo yote yatakayowasilishwa katika kigoda hicho yatafanyiwa utaratibu ili kuweza kutolewa kitabu kimoja cha mwalimu nyerere ikiwa ni sehemu ya kumuenzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, John Kalage amesema falsafa ya Mwalimu Nyerere ilijikita katika kutokomeza ujinga na Taasisi ya Haki Elimu wakishirikiana na Kigoda cha Mwalimu Nyerere wamedhamiria kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inakidhi matakwa ya sasa.