Na Suzana Uhiga, Bumbuli
RAIS Jakaya Kikwete amemtaka Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, asilazimishe kuwania nafasi ya urais kwa sababu wakati ukifika atapata.
Kauli ya Kikwete imekuja siku chache baada ya January kutangaza kuwania nafasi hiyo wakati akihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) wiki iliyopita.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga katika ziara yake, Rais Kikwete alisema licha ya kuwania nafasi hiyo, lakini pia January anapaswa kukubali matokeo ikiwa atapata au atakosa nafasi hiyo.
Rais Kikwete alisema kuwa mwaka 1995 wakati anawania nafasi ya urais kwa mara ya kwanza, alishauriwa kukubali matokeo ikiwa atashinda au atakosa nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa kura za maoni wa CCM.
“Nilipojaribu nilishindwa, lakini nilikubali matokeo kutokana na ushauri niliopewa na wazee akiwemo Mzee Thabit Kombo (mwanasiasa wa zamani wa Zanzibar),” alisema na kuongeza:
“Nasikia bwana mdogo, January unataka mambo makubwa, lakini mie hujaniambia, hata ulipogombea nafasi ya ubunge hukuniambia pia nilijua baada ya kushinda.
“Usilazimishe wakati ukifika utapata na hata ukikosa isiwe nongwa kubwa, sikiliza ushauri wa wazee kwani hata mimi mwaka 1995 nilifanya hivyo,” alisema Kikwete.
Pamoja na kutoa nasaha hizo, Rais Kikwete alisema January amejitahidi kuleta maendeleo kwenye jimbo lake katika kipindi kifupi alichokaa na hata kufanya kazi nzuri kwa kumsaidia kupitia wizara yake ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Alisema awali wakati yeye anaanza kazi alipangiwa Zanzibar wakati huo alikuwa na swahiba wake ambaye sasa ni marehemu, Sheikh Kombo kipindi hicho alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Afro Shirazi (ASP).
Alisema Kombo alikuwa anapenda kumueleza mambo mengi likiwamo la kumwambia awe na subira ya kuwania nafasi ya uongozi na kwamba kipindi chake kikifika atapata.
Alisema ushauri huo aliukumbuka ilipofika mwaka 1995 baada ya kuangushwa kuwania nafasi hiyo ndani ya chama.
“Kipindi hicho nilikuwa na kiu ya kuwatumikia Watanzania wenzangu lakini nilishindwa kupata nafasi hiyo kutokana na kuwa muda bado haujafika,” alisema.
Rais Kikwete alisema ilipofika mwaka 2005, aliendelea na dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo ambapo alibahatika kuwa Rais wa Tanzania, hivyo basi alimshauri January kufuata ushauri huo kwa sababu kila jambo lina wakati wake.
Mwanzoni mwa mwezi huu, January aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kugombea urais mwakani na kueleza kuwa amefikia uamuzi huo kwa asilimia 90.
January alitangaza dhamira hiyo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na BBC wiki iliyopita.
Mahojiano hayo yalikuwa yakirushwa kutokea London, Uingereza ambako yalifanywa na mtangazaji Salim Kikeke.
January alisema amekwisha kujitafakari, kujitathmini na ameridhika kwamba, wakati ukifika atachukua fomu za kugombea nafasi hiyo kupitia CCM.
Alisema kutokana na kujitathmini kwake, dhamira imemtuma kwa asilimia 90 kuwania kiti hicho akiwa na lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwatoa walipo.
January ni miongoni mwa makada wa CCM ambao kwa muda mrefu walikuwa wakitajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Uamuzi huo wa January uliibua mjadala mkali ambapo Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema uzee na ujana siyo sifa za mtu anayestahili kuwa Rais wa Tanzania atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Warioba aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na gazeti hili kufafanua habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), ikimkariri akisema rais ajaye anapaswa kuwa kijana.
Akifafanua, Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ameshangazwa na namna suala la uzee na ujana lilivyogeuzwa na kufanywa kuwa sifa mama ya mtu anayepaswa kuwa Rais ajaye kinyume na kile alichokizungumza wakati akihojiwa na gazeti hilo.
Jaji Warioba alisema anaamini jambo lililosababisha kukuzwa kwa ajenda hiyo ya uzee na ujana kwa sasa ni makundi ya urais.