29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

JK AMTUNUKU MWIGULU PHD YA UCHUMI

NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete,  amewatunuku vyeti wahitimu 4,757 wa  ngazi mbalimbali, akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu  Nchemba, aliyetunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi katika masuala ya fedha za kigeni.

Idadi ya waliotunukiwa shahada zao katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam jana, ni nusu ya wahitimu wote ambao ni 7,089 na kutokana na wingi wao wamelazimika kuhitimu kwa awamu mbili. Kundi jingine linatarajiwa kutunukiwa keshokutwa.

Mbali na Mwigulu kutunukiwa PhD katika mahafali ya chuo hicho ambayo ni ya 47, pia kulikuwa na wahitimu wengine 79 waliotunukiwa shahada hiyo katika fani mbalimbali.

Kikwete aliwapongeza walimu kwa kutoa wahitimu wengi wa kada hiyo kwa mwaka huu.

Pia aliwatunuku wahitimu 488 shahada ya umahiri na wengine 61 waliofuzu shahada ya uzamili, huku wahitimu 4,151 wakiwa wamefuzu shahada za awali.

Akizungumza kabla ya hafla hiyo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema wahitimu waliotunukiwa vyeti kwa awamu ya kwanza ni wa shahada za umahiri na uzamivu kwa Kampasi ya Mlimani ya Mwalimu Julius Nyerere na wahitimu wa shahada za awali kutoka kada ya uhandisi na teknolojia, kada ya habari na mawasiliano, kada ya sayansi asilia na tumizi.

Alisema wahitimu wengine ni kutoka kada ya sayansi na teknolojia za kilimo, kada ya jinsia, kada ya sayansi za jamii na Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano ya Umma, Shule Kuu ya Elimu. Wahitimu wa kilichokuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi watatunukiwa shahada zao Jumanne.

Alisema kwa kuzingatia uwiano wa jinsia kwa wahitimu wa mwaka huu, asilimia 30 ni wanawake na asilimia 70 ni wanaume.

“Tunawapongeza kwa dhati wahitimu kwa kutimiza vigezo stahiki vya kutunukiwa digrii katika fani na ngazi mbalimbali za uhitimu,” alisema.

Alisema anaamini wamewaandaa vya kutosha kujumuika na Watanzania katika kutafuta maendeleo. Pia wamewapa maarifa ya kuleta mabadiliko ya kuendeleza nchi na dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles