Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachofanyika Dodoma kesho.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana, zinasema moja ya ajenda kubwa inayoweza kutawala kikao hicho ni mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo limesusiwa na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa muda sasa Ukawa wamekuwa wakimtaka Rais Kikwete aliahirishe Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, kwa kile wanachodai kutotendewa haki.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kililiambia MTANZANIA kuwa kikao hicho cha siku moja kitajadili masuala mbalimbali likiwamo kufuatilia mwenendo wa makada wa chama hicho ambao katika siku za hivi karibuni kwa namna moja au nyingine wanadaiwa kutangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Nakwambia hakuna mjumbe hata mmoja anayejua nini kinakwenda kujadiliwa, Rais Kikwete amekwenda na siri nzito moyoni…tusubiri tuone nini kitatokea Dodoma.
“Hata hivyo, ajenda kubwa itakuwa uamuzi mpya juu ya hatima ya sasa ya Bunge Maalumu la Katiba ambalo mwenendo wake umekuwa ukilalamikiwa na wengi,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya CCM Makao Makuu.
Chanzo hicho kilisema kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kilichoanza juzi mjini Dodoma kufuatilia mwenendo wa makada sita waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa kuanza kampeni za kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati. Kikao hicho kitatoa taswira na mwelekeo mpya ndani ya CCM.
Uamuzi wa Rais Kikwete kuitisha CC unatokana na uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi Julai 16 mwaka huu ambayo ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
Kutokana na hali hiyo, CC iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao.
Julai 17 mwaka huu, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho inayotarajiwa kukutana Agosti mwaka huu ikibaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa watapoteza sifa ya kugombea.
Pamoja na adhabu nyingine, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya siasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mienendo yao ya siasa ikifuatiliwa.
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
Nape alisema CC ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina, kamati kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo,” alisema Nape.
Alisema kama itabainika makada hao hawakutekeleza masharti ya adhabu zao kama zilivyotolewa na CC, kuna hatari ya kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
“Kila mmoja anafuatiliwa mwenendo wake; kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo.
Kama watakuwa hawajatekeleza adhabu zao kamati itapeleka mapendekezo CC waweze kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na taratibu za chama,” alisema Nape.
Alisema ni muhimu kwa wanachama wote kukumbuka chama ni pamoja na katiba, kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga jambo ambalo halivumiliki.
Alisema nia ya CCM ni kusimamia na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu hasa katika kuelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Hoja ya kuendelea kufuatiliwa kwa makada hao ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, aliyesema amefungua jalada kwa ajili ya makada hao.
Suala jingine alilowasilisha Mangula ni ripoti ya ziara yake aliyoifanya katika mikoa ya Tabora na Kigoma na Tanga.
Februari 18 mwaka huu, CCM kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za nidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
MTANZANIA lilimtafuta Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye hakupatikana kwenye simu yake ya kiganjani na muda wote ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo, ofisa wa CCM Idara ya Uenezi alipoulizwa kuhusu kikao hicho cha CC alisema hana taarifa zozote kuhusiana na kikao hicho.
“Mimi sina lolote ninalolijua kwa sasa labla kwa kuwa nipo kwenye mapumziko acha nifuatilie taarifa zaidi. Lakini ninachojua hakuna kikao chochote kwa sasa,” alisema ofisa huyo.