29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI MAKABURI YANAVYOPOTEA VINGUNGUTI

\

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAISHA ya duniani huwa ni ya muda na yanapotoweka matokeo yake mtu huzikwa kaburini.

Kiimani watu huamini kwamba mtu anapokufa na kuzikwa roho yake haizikwi bali mwili wake tu.

Ndio maana watu wengi walio hai wamejijengea utaratibu wa kufuata mila na desturi fulani ili kuwaheshimu na kudumisha uhusiano mzuri na roho za watu au ndugu zao waliowatoka.

Wengi wamejiwekea utaratibu wa kudhuru makaburi wakiamini kwa kufanya hivyo wanakutana na kuzungumza na ndugu zao kwani licha ya kutengana nao kimwili bado huendelea kuamini kwamba kiroho wako pamoja.

Pia wako watu ambao wamejiwekea utaratibu wa kutenga maeneo rasmi ya kifamilia ya kuwazika waliotutangulia na makabila mengi hufika makaburini mara moja au mbili kwa mwaka kuyafagilia na kufanya ibada na matambiko.

Hivyo, makaburi yanatakiwa kubaki mahali maalumu penye kustahili faragha na heshima yake.

Hata hivyo, kwa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake maeneo ya kuzikia yamekuwa na changamoto nyingi.

Licha ya kuwapo kwa changamoto ya kujaa hasa katika maeneo maarufu ya kuzikia, changamoto nyingine ni kupotea kwa makaburi kutokana na sababu mbalimbali.

HALI HALISI VINGUNGUTI

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Kata ya Vingunguti ina watu 106,946.

Vingunguti ni kata ambayo ipo ndani ya Wilaya ya Ilala, Magharibi mwa Dar es Salaam.

Kwa muda mrefu ilizoeleka kuwa makaburi huweza kupotea kutokana na ama kuhamishwa kwa ajili ya kupisha shughuli zingine za kijamii kama ujenzi wa shule, hospitali au barabara lakini hili la Vingunguti linasikitisha.

Ukifika Vingunguti katika eneo la kuzikia lililoko Mtaa wa Miembeni jirani na Bonde la Butiama lazima utabaki na mshangao; kwamba unayoyaona ni makaburi au dampo la takataka.

Makaburi hayo sasa yanazidi kupotea na hata machache yaliyobaki nayo yako hatarini kutoweka.

Upande wa juu wa bonde hilo yanaonekana makaburi na katikati kuna njia inayolekea bondeni, lakini pembeni ya njia pia kuna makaburi ambayo yanaonekana yako nusunusu.

Kwamba zinaonekana alama tu zenye utambulisho wa marehemu husika (mawe na misalaba), lakini sehemu nyingine ya kaburi haionekani.

Mbaya zaidi katika eneo ambako sehemu ya makaburi imepotea pamegeuzwa dampo la kutupia takataka na hata alama chache zinazoonekana nazo ziko hatarini kupotea kabisa.

Hali hiyo inasababishwa na mmomonyoko wa udongo unaochochewa zaidi na mafuriko ya kila msimu wa mvua huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa.

Nyumba kadhaa zilizoko jirani na makaburi hayo nazo ziko hatarini kuanguka kutokana na mto kuzidi kusogelea katika upande wa makazi ya watu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembeni, Salehe Kibavu anawatupia lawama wananchi waliogeuza eneo hilo kuwa dampo la taka na wakulima wa mbogamboga.

“Nasisi wananchi tunachangia uharibifu wa mazingira kwa sababu kama kule chini (bondeni) unaona wale (anamwonyesha mwandishi) wanalima mboga na wengine wanachimba mchanga, matokeo yake mvua zikinyesha maji yanapoteza mwelekeo mto unazidi kusogea katika makazi ya watu,” anasema Kibavu.

Anasema wamekuwa wakielimisha wananchi kuacha kuchimba mchanga na kutupa taka katika bonde hilo lakini matukio mengine yamekuwa yakifanyika nyakati za usiku.

WANANCHI

Wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo wanasema kwamba kifo si mwisho wa maisha bali ni badiliko tu linalomwezesha mtu kuendelea na maisha mahali pengine hivyo ni vema makaburi hayo yakaheshimiwa.

“Yaani unaweza kupita hapa unakuta viungo vya watu vinazagaa na wakati wa mvua ukishuka huko chini unaweza kukutana na sanda au viungo vinasombwa na maji. Na hili tatizo si la leo tumeshalalamika mno.

“Wengi wetu tunaamini kwamba ndugu ama wazazi wetu walihama ulimwengu unaoonekana na kwenda ulimwengu usioonekana, yaani walihama ulimwengu wa wanadamu na kwenda ulimwengu wa roho ndio maana tumekuwa na utaratibu wa kuendelea kuwaheshimu.

“Kama mimi kila mwaka lazima niende nyumbani alikozikwa mama yangu kwa ajili ya kufanya dua ya kumwombea, huwa naenda kaburini kwake nasafisha kama msalaba umechakaa nabadilisha naweka mwingine,” anasema mkazi wa Miembeni, Salim Athumani (31).

Mkazi mwingine wa mtaa huo, Julieth Mwaipopo anasema maeneo ya makaburi yanapaswa kuheshimiwa na kuendelea kulindwa.

“Mbona yale ya Kinondoni wamejenga uzio au kwa sababu huku wanazikwa watu wa hali ya chini ndio maana wanayaacha?

“Mimi kwenye makaburi haya amezikwa dada yangu na kama kaburi halipo mimi naamini na yule mtu aliyezikwa pale hayupo, ni vibaya kwa sababu kama marehemu wakipuuzwa au kukasirishwa wanaweza kusababisha misiba, ugonjwa, umaskini na maafa mengine,” anasema Mwaipopo.

Mkazi mwingine wa mtaa huo Idrisa Mbakara, anaomba eneo hilo lilindwe ili kudhibiti utupaji taka.

“Yaani mimi naona kuliko kuzikwa hapa Dar ni afadhali ukazikwe nyumbani kwenu ulikozaliwa. Unaweza kushangaa makaburi yanahamishwa kwa shughuli zingine na mengine yamejaa lakini watu wanalazimisha kuzika,” anasema Mbaraka.

Naye Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa (CCM), ameomba jitihada za haraka zifanyike kunusuru makaburi hayo ili yasiendelee kupotea.

“Mimi binafsi eneo lenye makaburi naliheshimu mno tena naogopa hata kupita, hapa nimefika kwa taabu kwa sababu wananchi wangu wana tatizo. Makaburi yanazidi kupotea na hizi nyumba kama ikinyesha mvua kubwa zote zinaondoka yaani ni hatari tupu lakini bado watu wanaendelea kukaa,” anasema Kaluwa.

MANISPAA

Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu anasema makaburi hayo si ya manispaa bali ni ya jamii hivyo yenyewe ndiyo inawajibika kuyatunza.

“Jamii kama kanisa au msikiti inaweza kuamua ikawa na eneo lake la kuzikia, sisi tunakuwa tunayatambua maeneo ya aina hiyo lakini jamii husika ndio inawajibika kuyatunza.

“Kuna makaburi mengine yako pale karibu na machinjio ya Vingunguti ni ya jamii lakini watu walipoanza kuyageuza dampo la takataka Waislamu walijitokeza na kujenga uzio, hivyo na hawa wa Miembeni wachukue tahadhari ili makaburi ya ndugu zao yasiendelee kupotea,” anasema Shaibu.

Kwa mujibu wa ofisa huyo kwa makaburi yaliyo chini ya jamii kibali cha kuzikia huwa kinatolewa hospitalini lakini kwa yale ya manispaa kibali hutolewa na wao.

“Makaburi kama yale yaliyoko Karume au Buguruni yako chini yetu ndiyo maana tunawajibika kuyatunza,” anasema.

Kuhusu nyumba hizo anasema eneo hilo tayari ni hatarishi lakini wakazi wengi wa mabondeni wamekuwa wakikaidi kuhama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles