MISSOUR, Marekani
JIMBO la Missouri, limekuwa jimbo la kwanza nchini Marekani kuishitaki Serikali ya China kwa namna ambayo imeshughulikia janga la virusi vya ugonjwa wa corona.
Mashtaka hayo, yanakuja wakati ambao kuna ongezeko la matukio ndani ya Marekani kuinyooshea vidole vya lawama China kuhusu janga la corona.
Rais wan chi hiyo, Donald Trump mwanzoni aliisifu China kwa namna ilivyoshughulikia janga la virusi vya corona, lakini baada ya kuwa kwenye shinikizo kubwa kuhusu mlipuko huo, aliituhumu China kuwa ndio chanzo.
Hivi karibuni alitangaza kusitisha msaada wa fedha kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), akilishutumu kuipendelea China katika janga hili.
Wakati uchaguzi wa Marekani, ukitarajiwa mwaka huu, waangalizi wanasema mashtaka ya Missouri-sambamba na mashtaka mengine ya makampuni nchini Marekani,huenda ukawa mwisho wa kisiasa wa chama cha Trump cha Republican.
”Tunaona watu wengi wanatumia suala la China kufunika makosa ya serikali ya Marekani,” Tom Ginsburg, profesa wa masomo ya sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Chicago aliiambia Reuters.
China yenyewe haitakuwa na jambo la kuogopa kuhusu mashtaka hayo. Serikali za kigeni zinalindwa dhidi ya kushtakiwa katika mahakama za Marekani na kama Marekani ilitaka kuishutumu China, ingefanya hivyo kwenye majukwaa ya kimataifa.
Virusi vya corona vilipuka jijini Wuhan, China mwishoni mwa mwaka jana. Kufikia sasa Marekani ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi duniani 826,240.
Katika mashtaka hayo, Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la Missouri, Eric Schmitt aliituhumu China kuwa haikufanya jitihada za kutosha kudhibiti kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo.
Schmitt alidai wakazi wa jimbo hilo, wameathirika baada ya kupata hasara ya kiuchumi ya thamani ya mabilioni ya dola .
Lakini wataalamu wa masuala ya sheria, wana mashaka kuhusu namna jimbo hilo litakavyokwenda na mchakato wa hatua hizo za kisheria na msukumo zaidi kuhusu mchakato huo.
Mwanasheria mkuu anasema kwenye jimbo hilo, athari za corona ni kubwa.
“Familia zimetengana na wapendwa wao waliofariki kutokana.
”Hali ya uchumi ya wafanyabiashara wadogo ni mbaya, wengi wameanza kufunga biashara zao, na wale wanaoishi kwa ujira wa siku wanapata tabu kutimiza mahitaji yao ya chakula kila siku,”alisema.
Mpaka sasa jimbo hilo limethibitisha kuwa na wagonjwa 5,941 na vifo 189.
“Serikali ya China iliudanganya ulimwengu kuhusu hatari ya virusi vya Covid-19, ikanyawanyamazisha watu waliotoa taarifa kuhusu janga hili kwa mara ya kwanza na haikufanya jitihada za kuzuia kuenea kwa ugonjwa,”alisema.