NA RAYMOND MINJA, IRINGA
MWANAMUZIKI Judith Wambura ‘Jide’, amesema ili wanafunzi waishi maisha ya kifalme, wanatakiwa wajiamini katika kutimiza ndoto zao kupitia elimu.
Jide alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza wakati wa shindano la wanafunzi wa sekondari mkoani Iringa lililopewa jina la ‘I can think, I can Speak, Speech Competition 2016’.
“Wanafunzi hawatakiwi kukata tamaa katika masomo yao kwa kuwa wengi wenu mnapenda kuishi maisha ya kifalme, hivyo lazima mjiamini na mpiganie elimu ndiyo mje kuishi kama wafalme hapo baadaye,” alisisitiza.
Pia Jide amewataka wanafunzi kutokatishwa tamaa wanapohangaika kutimiza ndoto zao, kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutarudisha nyuma ndoto za kuwa na taifa la wasomi wanaojitambua.
“Katika kutimiza ndoto za kuelekea mafanikio, kuna changamoto nyingi mnazokumbana nazo, nawaomba msikate tamaa na msikubali kuambiwa hamwezi kutoka kwa watu wengine kwa kuwa mnaweza kufikia ndoto zenu kwa kujibidiisha kuzidisha juhudi na mafanikio mtayapata,” alisisitiza Jide.
Kwa upande wake Mratibu wa shindano hilo, Dickson Mseti, alisema lengo la shindano hilo ni kuwajengea wanafunzi uwezo na ujasiri wa kujieleza mbele za watu kwa lugha ya Kingereza.
Katika shindano hilo, Jofrey Tumaini aliibuka mshindi wa kwanza, Frank Kalongole wa pili na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Erick Rwelamila.