KHARTOUM, SUDAN
BARAZA la utawala la kijeshi la Sudan na muungano wa upinzani wameafikiana juu ya azimio la katiba litakalotoa fursa ya kipindi kipya cha serikali ya mpito.
Mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Mohamed Hassan Lebatt alitangaza makubaliano hayo jana, lakini hakutoa maelezo zaidi
Mkataba wa kugawana madaraka unaaainisha masharti ya kipindi cha miaka mitatu cha mpito yalikubaliwa mwezi uliopita na baraza la jeshi na viongozi wa upinzani.
Pia unataka kuwepo kwa serikali ya raia sita na majenerali watano.
“Ninatangaza kwa Wasudan , Waafrika na umma wa kimataifa kwamba wajumbe wa pande mbili wamekubaliana kwa ukamilifu juu ya azimio la katiba,” Lebatt aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa mikutano zaidi itafanyika kushughulikia masuala ya kiufundi ya sherehe ya kusaini, lakini hakutoa taarifa juu ya makubaliano yenyewe.
Shirika la habari la Reuters limeandika kuwa chini ya makubaliano hayo kikosi cha kijeshi chenye nguvu zaidi -Rapid Support Forces (RSF), ambacho kimekuwa kikishutumiwa kwa kuwauwa waandamanaji, sasa kitakuwa chini ya utawala wa jumla wa kijeshi
Pia huduma za ujasusi zitaongozwa na baraza la uongozi pamoja na baraza la mawaziri kwa ujumla.
Mkataba juu ya azimio unakuja baada ya baraza la kijeshi kutangaza kwamba wanajeshi wa RSF walikuwa wamefutwa kazi na kukamatwa kuhusiana na mauaji ya waandamanaji , wakiwemo watoto wanne wa shule waliouawa wiki hii.
Mauaji hayo yaliibua maandamano makubwa kote nchini humo na kusababisha kuchelewa kwa mazungumzo.
Hadi kufikia sasa pande hizo mbili tayari wamekubaliana yafuatayo:
Mgawanyo wa mamlaka utadumu kwa miezi 39
Baraza huru, baraza la mawaziri na bunge vitaundwa
Jenerali ataongoza baraza kwa miezi ya kwanza 21, na raia ataongoza miezi 18 iliyosalia.
Waziri mkuu, atakayeteuliwa na vuguvugu linalounga mkono demokrasia, ataongoza baraza la mawaziri
Mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya ndani watachaguliwa na jeshi.
Sudan imekumbwa na ghasia tangu jeshi lilipomng’oa madarakani rais Omar al-Bashir mwezi Aprili mwaka huu.
Mazungumzo yaliyochukua muda mrefu juu ya azimio yamekuwa yakifanyika huku ghasia zikiendelea.
Kusainiwa kwa mkataba wa azimio hilo lililosubiriwa kwa muda mrefu umeibua sherehe katika nchi ya Sudan , ambayo imekuwa katika limbo la mzozo uliodumu kwa miezi kadhaa.
Maandamano yaliibuka mwezi Desemba baada ya serikali ya Bashir kutangaza hali ya dharura ya hatua za kuunusuru uchumi .
Ni maandamano hayo hayo ndiyo yaliyosababisha kuondolewa madarakani na jeshi mwezi Aprili baada ya maandamanaji kubaki kwa muda mrefu nje ya wizara ya ulinzi mjini Khartoum.
Maandamano hayo yamekuwa ya kutaka mamlaka yahamishiwe mikononi mwa raia.