29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Jeshi la polisi, Tanroad Kagera waweka mikakati yakupunguza ajali Kagera

Nyemo Malecela, Kagera

Jeshi la Polisi mkoani Kagera kikosi cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na Tanroad limeweka mikakati kabambe kuhakikisha linapunguza ajali za barabarani hususan kwenye maeneo korofi ambayo ajali zimekuwa zikijirudia.

Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani mkoani Kagera (RTO), Denis Kunyanja amesema mikakati hiyo imepangwa katika makundi mawili ikiwemo ya muda mrefu na mfupi na imeanza kutekelezwa katika barabara ya Kibeta hadi Nyangoye ambayo imekuwa ikikabiliwa na ajali za mara kwa mara.

“Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na ukaguzi wa vyombo vya usafiri katika mifumo hatarishi ya breki, usukani na taili, na gari litakaloonekana halina dosari katika mifumo hiyo litawekewa stika ambayo itaonyesha kuwa lina ubora wa kufanya safari.

Tunakagua mifumo hiyo kwa sababu utengenezwaji wake unatumia gharama kubwa jambo linalosababisha wamiliki wa vyombo hivyo kushindwa kuvikarabati na kupelekea magari hayo kupata ajali,” alisema.

Kunyanja alisema pia Jeshi hilo limeweka askari maeneo ya Kibeta ambao watayakagua magari yote makubwa ya mizigo na abiria kwenye mifumo hiyo mitatu kabla ya kuanza kuteremka mlima Nyangoye na yakishamaliza mzunguko wa Rwamishenyi yatasimamishwa tena na kukaguliwa na askari kabla ya kumalizia kuteremka mlima huo.

Aidha Kunyanja alisema wamekaa na Tanroad ambao wamekubaliana waongeze alama za barabarani ili kuongeza tahadhari kwa madereva na watumiaji wa barabara hiyo.

Alisema tayari Tanroad wameandika maandishi ya tahadhari katika barabara hiyo yanayowataka madereva kutembea mwendo wa polepole, kuongeza matuta yatakayopunguza mwendo kasi pamoja na kuweka mabango makubwa ya kuwatahadharisha madereva kupunguza mwendo kasi.

“Pia Tanroad wanaendelea na mkakati wa kutafuta fedha ili waweze kuhakikisha wanapunguza mteremko huo kwa kuchimba kina cha barabara pamoja na kutanua barabara hiyo pembeni.

Na kwenye mzunguko wa Rwamishenye itawekwa nguzo kubwa itakayozuia magari yasiteremke chini endapo yatapata ajali maeneo hayo,” alieleza.

Kunyanja aliongeza kuwa taasisi hizo zimeendelea kushirikiana kutoa elimu ya matumizi bora ya barabara kwa watumiaji wote wa barabara wakiwemo madereva ili kupunguza sababu za kibinadamu kama vile uzembe wa kutotii sheria za barabarani unaosababisha ajali.

“Pia tanroad wameendelea kupambana na sababu za kimazingira kwa kujenga barabara ambazo zimekuwa na mashimo ambayo mengi yanasababishwa na mvua kubwa pamoja na utelezi barabarani,” alisema.

Kunyanja alisema mipango yote hiyo ni mwendelezo wa mipango ya mwaka jana ambayo ilisaidia kupunguza kiwango cha ajali kwa asilimia nne.

“Ukilinganisha takwimu za mwaka 2020 na 2021 tumefanikiwa kupunguza ajali mbili pekee ambazo ni sawa na asilimia nne tu.

Januari hadi Septemba, 2020 kulitokea ajali 29, kati ya hizo ajali 21
zilisababisha vifo wakati ajali nane zilisababisha majeruhi ukilinganisha na Januari hadi Septemba 2021 kulitokea ajali 27 ambapo kati ya ajali hizo 17 zilisababisha vifo wakati ajali 10 zilisababisha majeruhi,” alisema.

Kunyanja alisema mikakati hiyo inaenda sambamba na wiki ya usalama barabarani mkoani Kagera iliyozinduliwa Oktoba 27, mwaka huu wakati maadhimisho yake kitaifa yanatarajiwa kufanyika Novemba 11 mwaka huu mkoani Arusha.

Wakati naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Kagera, Wiston Kabantega alisema suala la kuthibiti ajali za mara kwa mara linahitaji ukaguzi wa kina kwa vyombo vya moto kwa kuwa licha ya ajali nyingi kusababishwa na makosa ya kibinadamu lakini pia ubovu wa vyombo vya moto navyo vimekuwa chanzo cha ajali kwa asilimia chache.

Alisema mikakati hiyo inaenda sambamba na wiki ya Usalama barabarani hivyo dhima kuu ni utoaji wa elimu kwa watumiaji wa barabara wote kwani wanayo haki ya kupata elimu hiyo ndio watafikia lengo la kuthibiti ajali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles