Na Malima Lubasha-Musoma
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma mkoani Mara, imemuhukumu Filbert Daud (38), jela miaka 23 baada ya kutiwa hatiani kwa makossa saba likiwemo la kujafanya Ofisa Mkaguzi wa Shule za Sekondari kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Akisoma hukumu hiyo ya kesi namba 12/2019, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jacob Ndira, alisema katika kosa la kwanza Januari mwaka huu mshtakiwa alikwenda kwenye Ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Mara na kujitambulisha kuwa yeye ni ofisa kutoka NECTA.
Kosa la pili ni kugushi barua ya NECTA iliyoonyesha kuwa inampa mamlaka ya kufanya ukaguzi katika Shule za Sekondari mkoani hapa, kosa la tatu, nne na la tano ni kujitambulisha kwa walimu watatu tofauti wa shule za sekondari kuwa yeye ni mkaguzi wa shule kutoka NECTA.
Katika kosa la sita na saba alidaiwa kuonyesha kitambulisho chenye majina tofauti na ya awali yaliyoonyesha kuwa yeye ni Athuman Salum kutoka wizara ya elimu.
Miongoni mwa shule anayodaiwa kufika ni Sekondari ya Nuru ikiyopo wilayani Serengeti, aliyodai kuwa ufaulu wa shule hiyo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2014 yalikuwa mabaya na kuhoji kwanini wanaajiri wageni kutoka nchini Kenya.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Isaka Ibrahimu, aliita mashahidi wanane na kielelezo cha barua ya utambulisho na kuomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili liwe ni fundisho kwa watu wengine.
Katika kusikiliza kesi hiyo, mshtakiwa hakuita shahidi yoyote bali alijitetea yeye mwenyewe, alipope wa nafasi na Hakimu Ndira kutoa utetezi wake kwa nini mahakama isimpe adhabu, alidai , ana mke na watoto wanne ana wazazi wote wanamtegemea huku mama yake akiwa amepooza.
Baada ya hakimu Ndira kupitia ushahidi wa pande zote mbili, alimuhukumu kifungo cha miaka 23 jela ili liwe fundisho kwa watu wengine.