TOKYO, Japan
WAZIRI mkuu wa nchi hii, Shinzo Abe, amesema kwamba, watakabidhi msimamo wao kuhusu suala la visiwa vya Kuril kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambaye alipendekeza kusainiwa mkataba wa amani ifikapo mwishoni mwa mwaka bila masharti yoyote.
Waziri Mkuu Abe alitoa taarifa hiyo juzi katika mdahalo wa Uchaguzi Mkuu na Waziri wa zamani wa Ulinzi, Shigeru Ishiba, uliorushwa na Kituo cha televisheni cha NHK.
Alisema kama alivyowahi kusema tangu mwanzo ni kwamba, ni lazima Rais Putin kwanza atafute suluhu ya matatizo hayo kitaifa na baada ya hapo ndipo mkataba huo utakaposainiwa.
“Nazidi kurudia kusema kwamba, Rais Putin kwanza shida ya taifa inapaswa kutatuliwa na baada ya hapo mkataba wa amani unaweza kusainiwa,” alisema Waziri Mkuu Abe.
“Nilijaribu kumweleza kabla ya Rais wa Urusi kutoa taarifa na nikarudia kufanya hivyo kabla ya kutoa mapendekezo,” aliongeza waziri mkuu huyo.
Alisema kwamba, wataalamu na wachambuzi wengi wanaamini kwamba, mapendekezo ya Rais Putin yanalenga kumaliza mgogoro huo kwa amani.