Na Mwandishi Wetu, Iringa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema kuanzia mwakani serikali itatoa maagizo kwa halmashauri zote kuhakikisha kila mwanafunzi wa darasa la kwanza anakwenda shuleni na mche mmoja wa mti siku ya kuanza masomo.
Pia kwa wanafunzi wa sekondari wanaoenda kuanza kidato cha kwanza nao watapaswa kwenda na miche mitatu wakati wa kuanza masomo yao.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akipanda miti na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlandege iliyopo Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa.
Alisema mwanafunzi atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba kwa shule za msingi na minne kwa sekondari na hatopewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake.
Alisema maagizo hayo anayatoa kwa kutumia kifungu cha sheria ya Mazingira Sura ya 191 ya mwaka 2004.
“Kifungu hicho kinasema waziri atakuwa msimamizi mkuu wa masuala ya mazingira na kwa mantiki hiyo atatoa miongozo muhimu ya sera ili kukuza, kulinda na kusimamia mazingira nchini Tanzania.
“Waziri anaweza kutoa miongozo ya jumla kwa wizara, idara za serikali, baraza, kamati ya taifa ya ushauri wa mazingira, jiji, manispaa, kamati ya usimamizi wa mazingira wa wilaya, wakala au asasi nyingine yoyote ya umma au binafsi, miongozo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutekeleza au kufanikisha yaliyoelezwa katika sheria hii,” alisema.
January alisema maelekezo hayo yatapelekwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha kuhitimu ni kukabidhi miti iliyopandwa wakati watakapoingia kuanza masomo na watahitajika kuitunza na kuihudumia katika kipindi chote cha masomo yao.
“Kuanzia Novemba 5 hadi 6, mwaka huu tutawaita wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti na mameya wote jijini Arusha kwa ajili ya kuwapa mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusiana na hifadhi ya mazingira, ikiwamo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji,” alisema January.
Katika hatua nyingine, alisema lengo la kushiriki upandaji miti na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe wa uhakika kwamba uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndiyo sababu hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.