26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

January Makamba hana kosa—Kinana

Abdulrahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana

Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amemkingia kifua Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba, kutokana na hatua yake ya kutangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kauli ya Kinana imekuja baada ya gazeti hili kumtafuta ili aweze kuzungumzia kitendo hicho ambacho kimetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni kuanza kampeni mapema kabla ya wakati, licha ya kupewa onyo na chama.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Kinana alisema hakuna makosa yoyote juu ya suala hilo na kusema kuwa kutangaza nia na kutaja vipaumbele si dhambi kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, isipokuwa dhambi ni kukusanya watu na kuwapa chakula pamoja na kugawa fedha.

“Ukisema kuwa mimi nitafanya kitu fulani na fulani si tatizo, sisi tulichokataza ni kukusanya watu na kuwaambia wakusaidie na kutoa fedha,” alisema Kinana.

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, jana alinukuliwa na vyombo vya habari akitangaza nia ya kuwania urais mwaka 2015 huku akisema kuwa ameshafikia uamuzi huo kwa asilimia 90.

Makamba alienda mbali na kutangaza vipaumbele vyake pindi akishika kiti hicho ambavyo ni pamoja na kushughulikia tatizo la ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora.

Alisema kuwa atahakikisha kila mwenye kipato cha chini anakuwa na kipato cha kati na mwenye cha kati atakuwa na cha juu.

Wakati Kinana akisema kuwa alichofanya Makamba si dhambi, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni wasaliti wakubwa ndani ya chama.

CCM pia ilitoa mwongozo na kanuni za uchaguzi ambapo, Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa CCM inawazuia wanachama kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.

Kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), ni kinyume kwa wanachama wake kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati.

Januari Mosi mwaka huu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wakati wa kukaribisha mwaka mpya alisema kuwa safari yake ya matumaini imeanza.

Alisema kuwa safari yake hiyo itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.

Kauli hiyo aliitoa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli Mjini bila ya kutaja safari hiyo ni ipi.

“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu,” alisema.

Mara baada ya kauli hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisisitiza juu ya wanachama wanaokiuka miiko na maadili kwa kuanza kampeni kabla ya wakati watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Itakumbukwa pia kuwa hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati akizindua filamu inayoitwa ‘I Love Mwanza’ alisema maneno ambayo pia yalitafsiriwa kuwa ni kuanza kampeni mapema.

Alisema kuwa “Kabla sijaja huku Mwanza, nilikwenda kwa Rais Kikwete kumuaga na kumueleza kusudio langu la kuja kufanya shughuli hii naye akanikubalia na kunipa baraka zote.

“Rais aliponikubalia, alinitaka nije huku haraka na baada ya kurudi jijini Dar es Salaam nikampatie taarifa za kile nilichokishuhudia jijini hapa.

Hapa siko peke yangu nimekuja na marafiki zangu wapendwa wanaoitwa Friends of Membe,” alisema Membe.

Kati ya watu waliokuwa wamefuatana na Membe ni pamoja na Waziri wa Maliasil, Lazaro Nyalandu, ambaye alisema “Rafiki yangu huyu nampenda sana na ni tarajio jipya kwa Watanzania…, kwa hiyo tumuunge mkono mimi nina imani naye, iko siku moja atakuwa kiongozi mkubwa wa taifa hili.”

Wakati akiwasili jijini Mwanza, Membe alipokewa na msafara wa vijana waendesha pikipiki zaidi ya 150 wakiwamo waliokuwa wamevaa tisheti za rangi ya njano zilizokuwa na maandishi mbele ya kifua yakisomeka, ‘Mheshimiwa Membe karibu Mwanza’.

Hata katika ukumbi wa Hoteli ya JB Belmont ulimofanyika uzinduzi huo, kulikuwa na bango lililokuwa na picha ya Membe yenye maandishi yaliyosomeka; ‘Tumaini la Watanzania’.

Ulipofika wakati wa harambee, Membe alinunua DVD moja ya filamu kwa Sh milioni nane.

Alinunua DVD nyingine kwa Sh milioni 1.5 aliyosema ni ya Rais Kikwete na pia alinunua nyingine mbili kwa ajili ya Makamu wa Rais, Mohamed Gharib Bilal (Sh milioni 1.4) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (Sh milioni 1.3).

Alisema kuwa, atakuwa baba wa pili wa wasanii baada ya Rais Kikwete ambaye pia anaitwa baba wa wasanii.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alishindwa kuthibitisha kama kweli Membe alitumwa na Rais Kikwete au la.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles